MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya
ya Arusha, Martin Muniss amemuomba Rais John Magufuli kulivunja Baraza
la Madiwani la Jiji la Arusha kutokana na kukosa uadilifu na kugeuka
kichaka cha siasa chafu.
Muniss alitoa ombi hilo wakati akifunga kikao cha Baraza Kuu la UVCCM
Wilaya ya Arusha na kueleza kuwa Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha
limekuwa na uonevu mkubwa katika maduka ya stendi ndogo na kubwa na
yaliyopo soko kuu kutokana na utaratibu uliotumika kuwa wa mashaka,
baada ya baadhi ya wafanyabiashara kunyang’anywa.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara walionyang’anywa vibanda hivyo
wamehusishwa na itikadi za siasa kwa CCM, hali aliyoeleza ni ukiukwaji
wa haki na ubaguzi mbaya katika taifa.
“Namuomba Rais Magufuli aiokoe Arusha, kwanza alivunje Baraza la
Madiwani wa Jiji, kutokana na serikali kupoteza mapato mengi huku
itikadi za siasa zikitangulizwa mbele, badala ya watu kufanya kazi za
kuwatatulia matatizo wananchi,” alieleza.
Alisema meya na madiwani wameshindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato
ya ushuru wa magari katika baadhi ya maeneo, badala yake wanaandaa
hujuma za kuipaka matope serikali ili ionekane utaratibu wa kurejesha
vyanzo vya mapato kutoka kwa wazabuni kuwa hauna faida.
Alisema uwepo wa madiwani katika Jiji la Arusha hauna manufaa yoyote
kwa sababu viongozi hao bila huruma, walisimamia wananchi wanaotumia
Soko la Kilombero kukatiwa maji kwa zaidi ya wiki tatu, soko ambalo
linahudumia nusu ya wakazi wa Arusha, hadi hapo aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya, Mrisho Gambo alipoamuru AWUSA warudishe maji.
Pia aliongeza kuwa viongozi hao wamegeuza Halmashauri ya Jiji kuwa
shamba la bibi la kuvuna fedha, baada ya kujiidhinishia viwango vikubwa
vya posho, ilihali wananchi wa kata ya Muriet wakikabiliwa na tatizo la
ukosefu wa maji na umeme huku wananchi wakichangishwa fedha za kujenga
barabara yao.