MKAZI wa kijiji cha Msati katika wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara,
Bahati Hunga (39), amehukumiwa na Mahakama ya mkoa wa Mara kutumikia
kifungo cha miaka 25 jela au kulipa faini ya Sh milioni 88, baada ya
kupatikana na hatia ya kukamatwa na vipande sita vya meno ya tembo
kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu, Adrian Kilimu baada ya
kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na waendesha mashitaka wa serikali,
Jonas Kaijage na Frank Nchanila kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari
24, 2014 akiwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh
800,000 katika eneo la kijiji cha Itiryo wilayani Tarime kinyume cha
sheria.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, waendesha mashitaka hao waliiomba
mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo ili kuwa fundisho
kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo na adhabu hiyo inaunga
mkono kaulimbiu ya serikali ya kuhakikisha wanyamapori wanalindwa kwa
nguvu zote dhidi ya majangili.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alipewa nafasi ya kujitetea na ndipo
aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu kwa sababu anayo familia
inayomtegemea.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kilimu alisema ameridhika pasipo kuacha
shaka dhidi ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa
mashitaka na ndipo akamhukumu kifungo cha miaka 25 jela au alipe faini
ya Sh milioni 88, ambako mtuhumiwa huyo alikosa faini hiyo na kwenda
jela kutumikia adhabu hiyo.