WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) imepiga marufuku usafirishaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa
ambapo mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo
ambavyo Serikali inavihitaji, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo
wake.
Imesema
zuio hilo linakwenda sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo
ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa,
pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini
na vijijini.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema
uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya maduhuli stahiki ya
rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.
Alisema
moja ya majukumu ya TFS, ni kuhakikisha inaanzisha na kusimamia
rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na
kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni kosa kuvuna hovyo
misitu na bidhaa zake bila kibali.
Mtendaji
huyo alisema kila zao linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru
stahiki na kukatiwa risiti, hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia
mbalimbali zinazokatazwa ni kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.
“Mazao
ya misitu, ikiwemo mikaa ni kosa kuuzwa na kusafirishwa bila kuwepo
kibali na risiti. Muuza mkaa lazima uwe na risiti, na wewe mnunuzi
tukikukamata na gunia la mkaa na huna risiti utawajibika.
“Tunataka
kuhakikisha maduhuli ya mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata
matumizi endelevu ya rasilimali za misitu hivyo ni biashara hii ya miti,
mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe wazi.
“Ni
marufuku kusafirisha mazao ya misitu usiku, kama mtu ana vigezo vyote
tunavyovihitaji kusafirisha mazao ya misitu anatakiwa kusafiri kuanzia
saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni, ikipita hapo, weka pembeni gari mpaka
asubuhi,” alisema.
Aidha
alisema TFS chini ya Wizara ya Maliasili ina Meneja miti kwenye kila
wilaya, ambao wanafanya kazi kwa karibu na Maofisa Watendaji wa vijiji
ambao hushirikiana kutoa vibali kwa kuvuna miti stahiki kisheria na
kutoa risiti.
Alisema
risiti hizo pamoja na vigezo vingine ikiwemo kuwa na usajili wa TFS,
leseni ya biashara na namba ya utambulisho wa mfanyabiashara (TIN), hati
ya kusafirisha mazao ya misitu humfanya mfanyabiashara kuruhusiwa
kuendelea na biashara ya mazao ya miti nchini.
Profesa
Silayo alisema TFS wataendelea na majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni
pamoja na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, alipozungumza na watumishi wa wizara hiyo mapema mwezi
uliopita.
Baadhi
ya maagizo hayo likiwemo la kupunguza vizuio kwenye maeneo mbalimbali
ya nchi, Silayo alisema wanafanya utafiti kujua kizuizi gani kitolewe na
kipi kibaki sambamba na kubana uvunaji holela wa misitu.
Alisema
lengo lao si kukamata magogo baada ya kuvunwa bali ni kuzuia misitu
isiharibiwe hivyo inapotokea, hutumia vizuio hivyo kukagua na kukamata
nyara hizo za serikali ili kuongeza maduhuli kwa mujibu wa sheria.
“Tumeanza
kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, ambayo kiuhalisia yana ukweli mkubwa
kwa hiyo tunataka kuondoa vizuizi visivyo na tija lakini pia
kuwasisitizia watu wetu kule vituoni kuzingatia weledi.
“Tayari
tumeanza kutumia mashine za kielektroniki za malipo yaani EFD kwenye
vizuio vyetu mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na tutaendelea
kuzisambaza maeneo mengine mara tu TRA watakapoziingizia program yao ya
malipo,” alisema.
Alisema
wana changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vitendea kazi hususan magari
lakini wanafanya jitihada mbalimbali kuhakjikisha wanazitatua ili misitu
iwe na mchango kwenye pato la taifa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali
Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo, alisema kitakwimu asilimia 94 za kaya
zote takriban milioni tisa nchini zinatumia mkaa kama nishani kuu, huku
maeneo ya mijini pekee ikiwa na asilimia 38 za watumia mkaa.
“Mahitaji
ya miti ni mita za ujazo 62.3 huku uwezo ukiwa ni mita za ujazo 42.8
hivyo uharibifu wa misitu unafika hekta 372,000 kwa mwaka sawa na
asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti,” alisema Kilongo.
Alisema
kwa takwimu hizo, miti na misitu nchini imekuwa ikipungua kwa kiasi
kikubwa na kusababisha uhitaji wa hekta mpya 185,000 za misitu
inayotakiwa kupandwa maeneo mbalimbali ya nchi.
“Upungufu
huu ni kichocheo cha uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya
hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za taifa hivyo suala
la kuilinda ni jukumu letu sote, kila gunia lazima lilipiwe ushuru,” alisema.
Pia
alisema katika jitihada za kurudisha misitu iliyopotea, upo mkakati wa
kitaifa wa kupanda miti ambapo kwa kila wilaya imepewa jukumu la kupanda
miti milioni moja na nusu kwa mwaka chini ya uangalizi wa Meneja misitu
wa wilaya husika.
Wiki
kadhaa zilizopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi
wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam, alisema nchi
inageuka jangwa kutokana na misitu mingi kukatwa kiholela huku maduhuli
ya serikali yakipotea.
Kauli
hiyo inaonekana kuanza kuzaa matunda baada ya TFS kuamua kuongeza kasi
ya usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki nchini kwa siku za hivi
karibuni hatua ambayo inadaiwa kuwa endelevu.