Sakata Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limezidi
kupanuka baada ya wanafunzi waliorudishwa nyumbani
kupinga kuitwa vilaza.
Jana wawakilishi wa wanafunzi hao ambao waliambatana na
viongozi wa
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), walisema wanapinga
pia hatua ya kutimuliwa chuoni.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Gibson Johnson alisema wanasikitika kuona
wanavyozushiwa tuhuma mbalimbali kuhusiana na wao kujiunga na chuo hicho.
Alisema wamekuwa wakijiuliza sababu za Serikali zinazotaka kuhalalisha kutimuliwa kwao chuoni
kuwa hawakuwa na sifa, jambo ambalo si la kweli.
“Siyo kweli kwamba sisi ni vilaza (wanafunzi wasiofanya vizuri darasani) na waliofeli na kupata
daraja sifuri.
“Sisi ni wanafunzi tuliofaulu kwa viwango vilivyohitajika kwa daraja la kwanza hadi la tatu na
tulipangiwa shule za kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, lakini tulibadili na kuamua
kujiunga Udom, hivyo tunaomba Serikali itumie busara zake.
“Hatuwezi kwenda kusoma kidato cha tano na sita kwa kuwa tumepoteza muda wetu.”
Alisema wanamshauri Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Rais John Magufuli kutumia
busara kuwarudisha chuoni kumalizia masomo yao.
Katibu Mkuu wa TSNP, Alphonce Lusako aliitaka Serikali ichukukue hatua kwa waliohusika
kudahili wanafunzi wasio na vigezo na kuwawajibisha.
“Lakini pia wanafunzi wafidiwe fedha na muda waliopoteza kwa wakati wote waliokuwa chuoni,
kama hawatapewa haki zao, sisi tutashirikiana na wadau wa elimu zikiwamo asasi za utetezi wa
kisheria kutafuta haki mahakama,” alisema Lusako.
Udom yazungumza
Ofisa uhusiano wa Udom, Beatrice Baltazali alisema wanafunzi hao wote walifaulu vizuri wakiwa
na daraja la kwanza, pili na wachache daraja la tatu.
“Wanafunzi wote walikuwa na nafasi ya kwenda kidato cha tano, lakini kwa kuwa waliahidiwa
ajira, waliona wapitie huku kwa kuwa watapata ajira ya moja kwa moja,” alisema.
Beatrice alisema walimu wa Udom walikuwa wanalipwa fedha za ziada kuwafundisha wanafunzi
wa programu hiyo kwa kuwa walikuwa wanatumia muda mwingi zaidi ya kiwango walichokuwa
wamepangiwa.
“Kutokana na madai ya malipo hayo, mkaguzi wa ndani aligundua kuna tatizo, ndiyo walimu nao
wakaamua kugoma, wanafunzi wakawa hawafundishwi Serikali ikaamua warudishwe nyumbani,”
alisema Beatrice.