MADUKA nane na bidhaa zilizokuwamo ndani yake,
yameteketea kwa moto uliozuka katika Soko Kuu
wilayani Nzega mkoa wa Tabora, baada ya kuanzia
katika moja ya vibanda.
Moto huo umeelzwa kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.
Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackline Liana
alisema moto huo uliteketeza vibanda pamoja na mali zote zilizokuwamo
ndani ya maduka hayo.
Liana alisema kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo itafuatilia ili kubaini
chanzo cha moto huo, na taarifa sahihi zitatolewa na mamlaka husika huku
tathmini ya hasara ya mali ikifanyika.
Aidha, Liana alisema jitihada za kuuzima moto huo zilifanywa na wananchi
pamoja na vyombo vya dola.
Aliwapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano katika majanga kama hayo.
Katibu wa wafanyabiashara wilaya ya Nzega, Githbet Kabamba alisema
sababu za kuzuka kwa moto huo ni hitilafu ya umeme katika moja ya vibanda
hali iliyosababisha moto huo kulipuka na kuanza kuunguza vibanda vingine.
Kabamba alisema jitihada za wananchi ndiyo zilizima moto huo baada ya jeshi la zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio, na hata lilipofika halikuwa na vifaa vya kuuzima.
Naye Kaimu Meneja wa Tanesco wilayani humo, Gerald Senya alisema kwa sasa hataweza
kuzungumzia moto huo hadi hapo watakapofanya uchunguzi.
chanzo: Nipashe