Wabunge
wa majimbo ya Mkoa wa Tanga wameahidi kujenga nyumba nne kwa ajili ya
makazi ya kaya ambazo ndugu zao waliuawa kwa kuchinjwa na watu
wasiojulikana katika kitongoji cha Kibatini, Jumanne ya wiki iliyopita.
Wakazi
hao walihamia katika eneo la Kona Z baada ya ndugu zao wanane kuchinjwa
na watu hao katika tukio linaloonekana kama kulipiza kisasi baada ya
wakazi hao kuwaripoti polisi watoto wanane walioonekana kwenye kitongoji
chao na kutiliwa shaka.
Wabunge
waliahidi kujenga nyumba hizo baada ya kukuta familia hizo zikiishi
katika mazingira magumu kwenye makazi yao mapya huku vyombo vyao
vikihifadhiwa uwanjani.
Walitoa ahadi hiyo jana walipokwenda kutoa rambirambi kwa familia hizo.
Wabunge
hao wote wakiwa wa CCM ni Adadi Rajabu wa Muheza, Jumaa Awesso na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu.
“Hii
haiwezekani, binadamu hawezi kuishi katika mazingira kama haya, hawa
wananchi wapo katika machungu ya kufiwa, inatia simanzi kuona wamehamia
huku, lakini hawana pa kuishi,” alisema Ummy ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu.
Alisema
wabunge wa mkoa wa Tanga kupitia CCM watajenga nyumba nne Kona Z kwa
ajili ya familia hizo, wakiwamo ndugu watatu wa familia moja ya marehemu
Issa Hussein aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji.
“Tumekubaliana
kwamba ujenzi huu utaanza mara moja wiki ijayo na tunataka nyumba
zikamilike haraka ili wafiwa hawa waondokane na adha ya kukosa makazi,” alisema Awesso ambaye ni Mbunge wa Pangani.
Awesso
aliitaka Serikali kuhakikisha inalinda maisha ya wakazi wa maeneo hayo
pamoja na kufanya uchunguzi utakaowezesha kuwanasa walioshiriki mauaji
hayo.
Wafiwa
hao waliwaomba wabunge kuvishinikiza vyombo vya ulinzi na usalama
kuweka ulinzi katika eneo hilo ili wasichinjwe watu wengine kwa kuwa
bado wana hofu kwamba wanaweza kufuatwa.
“Kama
mnavyoona tumekuja huku sisi kama tulivyo, tumeacha kila kitu Kibatini,
mazao mashambani na mifugo tumeamua kukimbia ili kuokoa maisha yetu kwa
hivyo tunakabiliwa na ukosefu wa chakula,” alisema Mwanaisha Hassan.