Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamtafuta mzee wa umri wa miaka
65 Dominick Kweka wa kijiji cha Kisereni wilayani Hai kwa tuhuma za
kumbaka msichana wa miaka 16 ambaye ni mtoto wa dada yake (Mjomba) na
kumpa ujauzito ambao sasa una umri wa miezi sita.
Akizungumza kwa njia ya simu kamanda wa polisi mkoani
Kilimanjaro Bw Wilbrod Mutafungwa amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na
kueleza kuwa juhudi za kumsaka zinaendelea ili afikishwe katika vyombo
vya sheria.
Bw Mutafungwa amesema, jeshi la polisi katika mkoa huo
halitavumilia kuona vitendo vya ubakaji vikiendelea kutokea kwa watu wa
aina hiyo ambao wanakatisha maandalizi ya maisha bora ya wanafunzi
wasichana.
Msichana huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule
ya sekondari ya Nkuu amesema, mjomba wake huyo alimbaka nyumbani kwake
wakati alimpopelekea sola kwa ajili ya kuichaji ili apate nafasi nzuri
ya kujisomea nyakati za usiku na ameiomba serikali aendelee na masomo
baada ya kujifungua.
Baba mzazi wa msichana huyo Bw Kilasauko Nyuki ameiomba serikali
imchukulie hatua kali za kisheria mzee huyo mwenye makazi katika kijiji
hicho na majiji ya Arusha na Dar es Salaam ambaye inadaiwa ametoroka
baada ya tukio hilo.
