HATMA ya kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya
aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC),
Daudi Mwangosi inasubiri uamuzi utakaotolewa kesho Jumatano (leo Juni 22) na Jaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Paul Kiwelo baada ya upande wa Jamuhuri na ule
wa utetezi jana kukamilisha kutoa ushahidi na utetezi wao.
Akitoa uamuzi huo leo baada ya maelezo
ya pande hizo mbili, Jaji huyo anayesikiliza kesi hiyo alisema; “Baada ya
kusikiliza shauri hili kutoka katika pande zote mbili naahirisha shauri hili
mpaka kesho saa 6.00 mchana nitakapotoa uamuzi kama mshatakiwa ana kosa la
kujibu au hana.”
Mwangosi
aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten aliuawa Septemba 2, 2012 katika
kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi Mkoani Iringa alipokuwa akiwajibika katika
kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kesi hiyo ambayo kila inapofikishwa
mahakamani hapo imekuwa ikiwaweka wanahabari katika mazingira ya kushindwa
kufanya kazi yao vizuri kutokana na vikwazo na vitisho wanavyopata kutoka kwa
askari Polisi wengi wanaouhudhuria kesi hiyo, inamkabili aliyekuwa askari wa
jeshi la Polisi, Pacificius Cleophace Simoni anayetuhumiwa kumuua mwandishi
huyo kwa kukusudia.
Awali wakili wa upande wa utetezi
Lwezaula Kaijage aliiomba mahakama hiyo imuachie huru mshatakiwa huyo kwa madai
kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri umeshindwa kumtia hatiani
mteja wake.
Kaijage alisema ripoti ya daktari
iliyowasilishwa mahakamani hapo na upande huo wa Jamuhuri haioneshi nani
aliyetenda kosa la mauaji hayo na kwamba ripoti hiyo inamuacha huru mteja wake
kwasababu inaweza kutumika kumfikisha mahakamani hapo sasa au baadae mtu yoyote
kuhusiana na kifo hicho cha Mwangosi.
Alisema ushahidi wa Jamuhuri umejikita
katika picha ya mauaji hayo iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la
Septemba 3, 2012 ambayo upande wao wa utetezi ulikataa usipokelewe mahakamani
hapo kama kielelezo cha ushahidi kwasababu upande wa mashtaka ulishindwa kupeleka
mahakamani hapo picha halisi iliyotumiwa na gazeti hilo na mpiga picha aliyepiga
picha hiyo.
Upande wa Jamuhuri unaowakilishwa na
mawakili wawili, Sandy Hyra na Ladslaus Komanya uliiambia mahakama hiyo kwamba ushahidi
uliotolewa sambamba na mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani hapo yanaonesha mtuhumiwa
huyo ana kesi ya kujibu.
“Upo ushahidi ambao hauwezi kwenda hivi
hivi bila mshtakakiwa kupata fursa ya kujitetea kabla ya hukumu ya kesi hii,”
alisema Wakili Komanya baada ya wakili mwenzake Hyra kutoa taarifa ya ushahidi
huo.
Hyra alisema Septemba 5,2012 mshtakiwa Pacificius
Cleophace Simoni alitoa ungamo kwa mlinzi wa amani na kukiri kuhusiaka na kifo
hicho.
“Baadhi ya maneno katika maungamo yake,
mshatakiwa alimwambia mlinzi wa amani kwamba anasikitika sana kusababisha kifo
cha marehemu,” alisema wakili huyo wa Jamuhuri.
Alisema maungamo hayo yaliyotolewa
mahakamani hapo kama kielelezo namba 3 cha upande wa mashtaka hayakuwa na
pingamizi lolote toka kwa mshtakiwa.
Katika maungamo yake, wakili huyo alisema
mshtakiwa huyo alisema akiwa na silaha
inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na ya machozi aliungana na askari
wenzake katika tukio hilo kwenda kutoa msaada kama ilivyochapishwa katika
gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.
Alisema ushahidi wa shahidi wao wa kwanza
unaonesha silaha hiyo ambayo matumizi yake ni lazima yafanywe na mtu inatumiwa
kupiga katika digrii 40 hadi 45 na sio kwa kuelekeza kwa mtu kama alivyofanya
mshatakiwa huyo.
Wakili huyo alisema aina ya kifo na
majeraha aliyopata marehemu yanadhihirisha kulikuwa na kusudio la mauaji hayo na
wala haikuwa bahati mbaya kwahiyo mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
“Shahidi wetu namba moja aliileza
mahakama kwamba maagizo yake kabla ya tukio hilo yalikuwa ni kuwatawanya
waandamanaji. Mwangosi aliuawa baada ya waandamanaji kutawanya na hakukuwa na
amri yoyote ya kutumia silaha dhidi ya Mwangosi,” alisema.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo askari Polisi zaidi ya 30 waliokuwepo mahakamani hapo, walimchukua kwa kasi mtuhumiwa huyo na kumkimbiza katika magari mawili ya Polisi aina ya LandLover yaliyokuwepo mahakamani hapo na kutokomea naye huku wanahabari wakibuguziwa na baadhi yao wakizuiwa kumpiga picha mtuhumiwa huyo.