KUNDI la wanaharakati sasa linataka masomo kuhusu ngono yakaguliwe na Wakenya kabla ya kuruhusiwa kufundishwa shuleni.
Kundi hilo linalojulikana kama Sauti ya Wanjiku
Jumapili lilisema kuwa masomo hayo yanajumuisha masuala yanayokiuka
maadili ya Wakenya.
“Silabasi kuhusu masuala ya ngono iliandaliwa na
mashirika ya kigeni bila kuzingatia maadili yatu ya kiafrika. Baadhi ya
masuala yaliyomo kwenye silabasi hiyo ni namna watoto wa kuanzia umri wa
miaka sita wanaweza kutangamana na wenzao ambao walibadilisha jinsia au
wanajihusisha na ushoga,” akadai mshirikishi wa kundi hilo Dkt Francis
Kuria.
Kwa mujibu wa wanaharakati hao waliokuwa wakihutubia
wanahabari jijini Nairobi, serikali ilikubali kufundisha wanafunzi
silabasi hiyo kwa lengo la kutaka ufadhili kutoka kwa mataifa ya kigeni.
“Wakenya hawakuhusishwa katika maandalizi ya masomo
hayo ambayo huenda yakahatarisha maadili ya watoto shuleni. Hatuwezi
kuruhusu mataifa ya Magharibi kutuamulia masuala yanayopaswa kufundishwa
shuleni ,” akasema Dkt Kuria.
Kulingana na wizara ya Elimu, masomo kuhusu ngono
inalengakukabiliana na visa vya watoto kupata mimba za mapema na
kujizuia kutokana na maradhi ya Ukimwi.
Wanaharakati hao pia walishutumu wizara ya Elimu na
Taasisi ya Uendelezaji wa Mtalala nchini (KICD) kwa kutohusisha wananchi
katika maandalizi ya mfumo mpya wa elimu wa 2-6-3-3-3 unaotarajiwa
kuchukua mahali pa 8-4-4.
“Mswada wa mfumo mpya unafaa kuwekwa wazi ili uweze
kukaguliwa na Wakenya badala ya kuhusisha washikadau wachache pekee
katika mahoteli ya kifahari. Katiba inahitaji kuwa wananchi wanahusishwa
kikamilifu katika maamuzi muhimu hivyo, Wakenya ni lazima washirikishwe
katika mfumo mpya wa elimu,” akasema Dkt Kuria.
Kongamano la wataalamu
Mnamo Machi, zaidi ya wajumbe 500 wakiwemo wataalamu
wa kimataifa walikongamana jijini Nairobi kujadili mtalaa mpya ambao
umekuwa ukiandaliwa na taasisi ya KICD kwa muda wa mwaka mmoja sasa.
“Hatupingi kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Elimu lakini
tumegundua baadhi ya watu walipenyeza baadhi ya masuala yasiyofaa katika
silabasi hivyo tunataka Wakenya wote kutoa maoni yao kabla ya kuanza
kutekelezwa,” akasema mwanachama wa Sauti ya Wanjiku Bi Anne Musomba.
Kulingana na Waziri wa Elimu Fred Matiang’i, mfumo mpya wa elimu unatarajiwa kuidhinishwa na kongamano la kitaifa Julai.