POLISI nchini Burundi Ijumaa waliwakamata wanafunzi 11 wa shule moja ya upili kwa kuharibu picha ya Rais Pierre Nkurunziza.
Mamlaka nchini humo zilisema kuwa watu watatu walipigwa risasi katika maandamamo dhidi ya kiongozi huyo.
Ripoti zilisema kuwa wanafunzi hao walifunguliwa mashtaka baadaye katika mahakama moja mjini katika eneo la Muramya.
“Kiongozi wa mashtaka ameamua kuwazuilia wanafunzi 11
kwa kumtukana kiongiozi wa nchi,” akasema afisa mmoja wa polisi ambaye
hakutaka kutajwa.
“Wanafunzi hao; wasichana sita na wavulana sita
walizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Muramvya mwendo wa saa sita za
mchana,” akasema.
Habari hizo zilithibitishwa na watu kadhaa, ikiwa ni pamoja na mzazi mmoja aliyemwona binti yake akipelekwa katika kituo hicho.
Mawakili kadhaa pia walithibitisha kukamatwa kwa wanafunzi hao.
Kulingana na sheria za nchi hiyo, shtaka la kumtusi rais lina hadi kifungo cha miaka 10.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa wenyewe yalizuka
nchini humo mnamo Aprili 2015 baada ya Rais Nkurunziza kutangaza kwamba
angewania katika kipindi cha tatu cha urais.
Kiongozi huyo alitajwa mshindi kwenye uchaguzi ambao ulifanyika mwezi Julai, licha ya upinzani kukataa kushiriki.
Hadi sasa, ghasia hizo zinakisiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 500, huku wengine 270,000 wakiachwa bila makao.
Polisi walisema kwamba wanafunzi hao walikamatwa Ijumaa na kikosi maalum cha usalama wa taifa.
Maandamano ya amani
Baada ya kisa hicho, mamia ya wanafunzi katika Shule
ya Upili ya Muramvya walifanya maandamano ya amani huku wakitaka wenzao
kuachiliwa.
“Polisi katika kitengo maalum cha usalama walifyatua risasi ili kuwatawanya waandamanaji,” zilieleza duru.
Wanafunzi wawili walijeruhiwa katika tukio hilo.
Katika kisa kingine tofauti mwezi uliopita, zaidi ya
wanafunzi 300 wenye umri wea kati ya miaka 14 na 16 walifukuzwa shuleni
baada ya picha ya rais kupatikana ikiwa imeharibiwa katika mojawapo ya
vitabu vyao. Tukio hilo lilifanyika katika mji wa Ruziba.
Mji huo ni ngome ya kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa.
Katika baadhi ya picha hizo, macho ya rais yalikuwa yametolewa, huku kukiwa na maandishi ya kumtusi.
Rais Nkurunziza amekuwa akipinga visa vyovyote vya
matumizi ya nguvu dhidi ya raia. Nchi kadhaa za Magharibi zimetishia
kukomesha utoaji misaada kwa taifa hilo ikiwa halitakoma kuendeleza
ukatilo dhidi ya raia, hasa katika ngome za upinzani.
Mapema 2016, Ubelgiji ilikatiza uhusiano wa
kidiplomasia pamoja na utoaji misaada kwa serikali ya Rais Nkurunziza
hadi pale mgogoro wa kisiasa utashughulikiwa na muafaka ufaao wa
makubaliano kuafikiwa.