Washtakiwa sita wanaokabiliwa na makosa tofauti yakiwemo ya kubaka,
kulawiti na kusambaza picha chafu na za ngono wameendelea kusota rumande
kwa kukosa dhamana, baada ya mvutano mkali wa mawakili wa upande wa
mashtaka na upande wa washtakiwa kuibuka mahakamani hapo, na hakimu
anayesikilisha shauri la dhamana kuahirisha shauri hadi Juni 15 mwaka
huu kutoa uamuzi juu ya dhamana.
Miongoni mwa washtakiwa hao, wawili,Iddi Adam Mabena (21) mkazi wa
Njombe na Zuberi Thabit (30) mkazi wa Mbarali Mbeya wanaokabiliwa na
shtaka la kumbaka na kumlawiti binti mwenye umri wa miaka 21 mkazi wa
Wami Dakawa,wilayani Mvomero wanalodaiwa kutenda Aprili 27 mwaka huu
majira ya usiku katika nyumba ya kulala wageni ya titii iliyopo wami
dakawa wilayani mvomero,shauri lao linalosikilizwa faragha limeahirishwa
tena mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Morogoro
Mary Moyo.
Upande wa mashtaka katika shauri hilo linalosikilizwa faragha kwa
mujibu wa sheria, umewakilishwa na waendesha mashtaka Gloria
Rwakibalila, Edgar Bantulaki, Calistus Kapinga na Mohamed Mkali na
limepangwa kufikishwa tena mahakamani hapo Juni 15 mwaka huu kwaajili ya
kuanza usikilizwaji wa awali baada ya upelelezi kukamilika.
Uamuzi wa dhamana itolewe ama isitolewe umeshindwa kufikia muafaka
baada ya mvutano wa kisheria wa mawakili wa utetezi na wa Jamhuri,
katika shtaka la kusambaza picha chafu na za ngono kwa njia ya mtandao
kinyume na sheria ya makosa ya mtandao no 14 ya mwaka 2015,
linalosikizwa mbele ya hakimu Ivan Msaki,wa Mahakama ya Hakimu mkazi
mkoa wa Morogoro,dhidi ya washtakiwa sita,iddi Mabena na Zuberi
Thabit,wanaotetewa na wakili Mohamed mkali,na Rajab Salehe,Ramadhani
Ally Makunja, Muhsin Ngai na John Peter Thabiti maarufu kama paroko,
wakazi wa wami dakawa wilayani Mvomero wanaotetewa na wakili Ignas
Punge.
Upande wa mashtaka umeendelea kutetea uamuzi wake wa kuwasilisha
kiapo cha kupinga dhamana kwa vile shauri hilo limevuta hisia ya watu,
usalama wao utakuwa mashakani wawapo uraiani hasa ikizingatiwa
wanadaiwa kudhalilisha utu wa mwanamke na kutoharibu upelelezi kwa vile
bado haujakamilika,na kwamba taarifa za kiintelijensia zimebainisha
wakiachiwa huru wanaweza wakadhuriwa na jamii.
Hata hivyo upande wa utetezi uliowasilisha hati kupinga kiapo hicho
umedai dhamana ni haki ya mshtakiwa,hakuna raia aliyewasilisha kiapo
kuhusu hasira kali alizonazo dhidi ya washtakiwa isipokuwa labda ni
hisia za mkuu wa upelelezi wa mkoa.
Hakimu Ivan Msaki ameahirisha shauri hilo hadi Juni 15 mwaka huu
ambapo uamuzi wa washtakiwa kupewa dhamana au kunyimwa dhamana
utajulikana.