Mkazi wa Kijiji cha Ussonge, Kata ya Nyandekwa, Mkungu Kodoli (50)
amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora
akikabiliwa na mashtaka ya kumuua mkewe.
Akimsomea mashtaka jana
mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ajali Milanzi, Mwendesha Mashtaka wa Polisi,
Frank Matiku alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 26, mwaka
huu saa 4.30 usiku nyumbani kwake.
Matiku alidai kuwa mshtakiwa alimpiga mkewe, Nsungurwa Dotto (46) kwa fimbo kichwani na kusababisha kifo chake.
Alidai chanzo cha mauaji hayo ni baada ya mshtakiwa kumfumania mkewe akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.
Mwendesha
mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na
kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu kitu chochote kwa
sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za mauaji
hadi atapofikishwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.
Matiku alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Milanzi kuiahirisha hadi Juni 14, itakapotajwa tena.