Watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti, akiwamo aliyeuawa kwa kipigo na kuchomwa moto kwa tuhuma ya kupora simu ya mkononi aina ya Tecno.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema Juni 2, mtu huyo ambaye
jina lake halikupatika anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25
hadi 30, aliuawa baada ya kumpora simu mpitanjia eneo la Ngaza, Kata ya
Nyegezi jijini Mwanza.
“Kabla
ya kupora simu mtu aliyejulikana kwa jina la Aanicia Rwezaura alitishwa
na yule aliyeuawa kwa panga, lakini wananchi wenye hasira kali
walimwandama, kumpiga na hatimaye kumchoma moto hadi kufa,” alisema Kamanda Msangi
Katika
tukio jingine, kamanda huyo amesema watu wawili wamefariki dunia na
wengine wanne kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha
Isunganh’olo wilayani Sengerema.
Aliwataja
waliofariki kuwa ni dereva wa gari aina ya Toyota Prado, Samson Kasala
na mwendesha baiskeli, John Manyilizu aliyekuwa akipita pembezoni mwa
barabara.
“Gari hilo lililokuwa kwenye mwendo kasi lilipasuka gurudumu na kuacha njia kabla ya kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi,” alisema Msangi
Waliojeruhiwa
katika ajali hiyo ni Mandago Misana, Thobias Kitenge, Jesca Andrew na
Mehob Peter ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa
matibabu.
Kamanda
Msangi aliwataka madereva kuwa watulivu barabarani na kuzingatia sheria
za usalama barabarani na kuwaonya wale wasiozizingatia kwamba watabanwa
kisheria.
Alisema mwendokasi umekuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani ambazo iwapo wahusika wangekuwa makini zingeweza kuepukika.