Watu 9 Waachiwa Huru Mauaji Ya Watu Watatu Msikitini Jijini Mwanza

Watu 9  kati ya 14 waliokuwa wameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea katika msikiti wa Rahman, Mkolani jijini Mwanza wameachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia.

Akizungumza na nyumbani kwao mtaa wa Nyanghingi jana, mmoja wa watu hao, Hamidu Said (31) alisema akiwa na wenzake tisa, waliachiwa Mei 30 baada ya kuonekana hawahusiki katika tukio hilo.

Said alikamatwa Mei 18, muda mfupi baada ya kufika eneo la tukio kushuhudia mauaji hayo.

“Kati ya watu tisa tulioachiwa, wanaume tulikuwa watano, wanawake wawili na watoto wawili mmoja akiwa na miaka 13, mwingine 16,” alisema Said.

“Sikuamini kama natoka rumande, ila namshukuru Mungu kwa jinsi alivyonitetea hadi kuona sina hatia,” alisema.

Akizungumzia tukio la mtoto wake kukamatwa, baba wa Hamidu, Said Bahebe, alisema ni vigumu kuelezea mshtuko na machungu waliyoyapata baada ya kijana wao kukamatwa na polisi, hivyo alilazimika kumuombea dua kwa kuachiwa baada ya kukutwa hana hatia.

Alisema kama ambavyo hawakuamini siku waliposikia kijana wao amekamatwa wakati ameenda kushuhudia tukio, kadhalika hawakuamini kuona anaruhusiwa kurudi nyumbani.

“Hatukutegemea kama angetoka ndani mapema,” alisema.

Bahebe alisema kwa siku 13 alizokaa rumande kijana wake, familia haikuwa na amani na ilikosa raha wakidhani ataishia jela.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahamed Msangi alisema wamewaachia watu hao ambao walionekana hawana hatia, lakini bado wanafuatilia wengine ambao wanaonekana kuhusika na tukio hilo bila ya kutaja idadi ya watu waliochiwa.

“Wapo baadhi walioachiwa, wengine watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya kuona ushahidi una kila aina ya dalili za kuhusika na tukio hilo,” alisema Msangi.

Katika mauaji hayo, watu watatu waliuawa kwa kukatwa mapanga wakiswali msikitini akiwamo Imamu wa Msikiti wa Rahman, Feruz Ismail (27), Mbwana Rajab (40) na Khamisi Mponda (28).

Ilielezwa kuwa kabla ya kuanza kuwashambulia waumini kwa mapanga, wavamizi hao waliamuru watoto waliokuwamo msikitini humo kutoka nje kupitia mlango wa nyuma unaotumiwa na wanawake.

Katika tukio hilo, mtoto Ismail Abeid (13) alinusurika baada ya kupita kwenye mlango mwingine, tofauti na ule ambao wavamizi walielekeza utumike ambako walijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga vichwani walipopita.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo