Wafanyabiashara wa sukari katika maduka ya reja reja
wameandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani
Manyara, Crispin Meela wakipinga kuuziwa mfuko wa sukari wa
kilo 25 kwa Sh110,000.
Wakizungumza jana nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,
walisema kuna mfanyabiashara mmoja (jina tunalihifadhi)
anawalazimisha kununua sukari kwa bei hiyo pamoja na biskuti boksi tano.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Victor Malele alisema wameshangazwa kutakiwa kulipia biskuti
wakati mahitaji yao ni sukari.
“Analazimisha tuchukue na biskuti, ndiyo sababu tumepinga. Na
kama ukikataa biskuti hakuuzii sukari,” alisema Benjamini Musa.
DC aagiza kukamatwa
Akizungumza baada ya kupokea ujumbe wa wafanyabiashara hao, Meela aliagiza kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kwa madai ya kuuza sukari hiyo kinyume cha bei elekezi ya Serikali.
Hadi kufikia jana, maduka mengi ya mji wa Babati hayakuwa na sukari na yaliyokuwa na bidhaa
hiyo yaliuza kwa Sh3,000 hadi 6,000 kwa kilo moja.
Mfanyabiashara huyo anashikiliwa kwa mahojiano na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA)
Mkoa wa Manyara kwa tuhuma hizo.
“Akimaliza kuhojiwa TRA nimetoa maelekezo apelekwe polisi, hatuwezi kuvumilia mtu mmoja
kuwapa shida ya sukari wananchi wetu, ingawa ni kweli hatuna sukari ya kutosha katika mji,”
alisema.
Katika mji wa Babati kwa takriban siku tatu, hoteli nyingi zimekuwa zikisitisha kuuza chai
kutokana uhaba wa sukari.