Mchungaji wa Kanisa la Hopran Mission
lililopo Tabata Kinyerezi, Jimmy Kapenye (42) amehukumiwa
kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh2m baada
ya kupatikana na hatia ya kutapeli Sh13.7m, mali ya askofu wa
kanisa hilo.
Kapenye amekuhumiwa kifungo hicho leo katika mahakama ya wilaya ya Ilala ambapo mbali na kifungo hicho, mchungaji huyo
ametakiwa kulipa fidia ya Sh13.7m alizotapeli.
Mchungaji huyo anadaiwa kupewa mahindi na alizeti yenye thamani ya Sh13.7m na askofu wa
kanisa hilo, Charles Nicholas kwa ajili ya kuuza na fedha itakayopatikana itumike kulipa mkopo
wa trekta ambalo waumini walikopeshwa na Suma JKT. Hakufanya hivyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Wilaya ya Ilala, Maua Hamduni amesema mahakama yake
imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka waliotoa dhidi ya mshtakiwa huyo.
“Kutokana na ushahidi ulitolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, mahakama
inakuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh2m na kulipa fidia ya Sh
13.7milioni ili liwe fundisho kwa watu wote wenye tabia kama hizi ambao ni viongozi wa dini,”
alisema Hakimu Hamduni.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwanini
asipewe adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela na mshtakiwa huyo alijitetea kuwa
apunguziwe adhabu kwa kuwa ana maradhi ya tezi dume na ana familia inayomtegemea.
