Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha
amezuia maandamano yaliyoitishwa na Chama cha Walimu
nchini (CWT) wilayani hapa, ambayo yalipangwa kufanyika leo
kwa kuwa hayana msingi wowote.
Mwenegoha ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya amesema hoja zote 17 ambazo
waliziorodhesha walimu zilishajibiwa na mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kupitia barua yenye
Kumb. Na. A.30/3/84 ya tarehe Mei 16, mwaka huu.
Mkuu wa wilaya amekitaka chama hicho kama hakikuridhishwa
na majibu hayo wakutane tena na mkurugenzi kuzungumzia masuala hayo, badala ya kufanya maandamano.
Amesema maandamano hayo yataathiri shughuli za mitihani ya “mock” kwa kidato cha nne
inayoendelea kati ya Mei 10 na Mei 20, mwaka huu na ile ya “Step” chini ya BRN kwa shule za
sekondari iliyoanza Mei 16 na kukamilika Mei 20, mwaka huu.
Amesema kamati ya ulinzi na usalama iko imara kuyadhibiti maandamano hayo na vitendo
vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika wilaya hiyo.
