Askari Polisi afikishwa mahakamani kwa kupokea mishahara miwili

Jeshi la Polisi mkoani Kagera katika kukabiliana na sakata la watumishi hewa ndani ya Jeshi hilo limemfikisha mahakamani askari mwenye namba H.1218 aliyekuwa mtumishi wa jeshi hilo wilayani Ngara aliyetajwa jina la Mungelule Alex kwa tuhuma ya kupokea mishahara miwili iliyokuwa ikiingizwa kwenye akaunti yake iliyoko kwenye benki ya NMB kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2016.

Mtuhumiwa  akiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi amefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa wa Kagera, Denis Mpelebwa na kusomewa mashtaka dhidi yake na Hashim Ngole ambaye ni wakili wa serikali mkuu mfawidhi wa mkoa wa Kagera.
 
Akisoma mashtaka mheshimiwa Ngole ameiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alianza kupokea mishahara miwili tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2016 akiwa mtumishi wa serikali ambapo katika kipindi hicho amejipatia zaidi ya shilingi milioni kumi na tano. 
 
Awali kamanda wa jeshi la Polisi Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Augustine Ullomi akizungumza amesema jeshi la polisi litaendelea kuwachukulia hatua za kisheria askari wanaofanya kazi kinyume na maadili ya utumishi wa umma, amesema hatua ya kumfikisha mahakamani askari aliyekuwa anakula mishahara miwili ni onyo kwa askari wengine.
 
Mtuhumiwa huyo amerudishwa rumande baada ya wadhamini wake waliojitokeza kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa na mahakama, kesi ya mtuhumiwa huyo itatajwa tena mei, 2 mwaka huu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo