Mbunge wa Meatu mkoani Simiyu, Salum Hamis, amemwomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumwondoa mwekezaji katika pori la akiba la Makao, wilayani hapa.
Mbunge huyo amemtaka Majaliwa kumwondoa mwekezaji huyo anayemiliki kampuni ya Mwiba Holdings ambaye alidai amekuwa akiwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga na wengine kuwasababishia ulemavu kwa kisingizio kuwa wanaingiza mifugo katika pori hilo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika uwanja wa Kituo cha Magari ya abiria cha mjini Mwanhuzi juzi, Salum alisema kero ya kwanza ambayo ni jipu kubwa ni mwekezaji huyo.
Mbunge huyo alisema mwekezaji huyo amekuwa akiwatesa wananchi kwa vipigo na baadhi kupata vilema vya maisha na kuiomba serikali kuchukua hatua zinazostahili dhidi yake.
Alisema amekuwa akitumia fursa hiyo ya kuwanyanyasa wananchi hasa wafugaji ambao wanaishi kando kando mwa hifadhi ya Pori la Akiba la Maswa na kutumia helkopita kuswaga ng’ombe na kusababisha kuvunjika miguu.
Akitokwa na machozi mbele ya Waziri Mkuu, mbunge huyo alielezea waziwazi kero wanazozipata wananchi wa wilaya ya Meatu, wakiwamo wa jimbo lake la uchaguzi.
Alisema wakati umefika kwa serikali ya awamu ya tano kushughulikia kikamilifu kero za wananchi wake akiwamo mwekezaji huyo.
“Amekuwa akitumia helkopita yake kufukuza mifugo iliyoko maeneo jirani ya mwekezaji huyo na kisha baadhi ya mifugo kuingia ndani ya hifadhi na kuikamata na kuwatoza Sh. 500,000 kama faini ya mifugo kuingia ndani ya hifadhi. Huko ni kuwaonea wananchi,” alisema.
Akijibu suala hilo, majaliwa alisema kulingana na hali halisi alijionea wakati mbunge huyo akiwasilisha hoja yake na kamwe serikali haiwezi kumuonea haya mwekezaji huyo akiendelea kufanya vitendo vibaya na viovu kwa wananchi pasipo kuheshimu sheria za nchi.
Majaliwa alikubali kulishughulikia mara moja suala hilo na kumwaagiza Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo, kukutana na mwekezaji huyo na kupitia mikataba yote.
“Mkuu wa Mkoa nakuagiza ukutane na mwekezaji huyo na mpitie mkataba wake na kisha niipate na taarifa hiyo ofisini kwangu Machi 11, mwaka huu. Iwapo itabainika kuwa amekiuka baadhi ya vipengele katika mkataba wake, kuna hatari ya kufutiwa vibali vya uwindaji” alisema.