Aliyekufa muda mchache kabla ya ziara ya Waziri Mkuu aacha vilio

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemlilia aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Trasias kagenzi, aliyefariki dunia juzi.
 
Kagenzi alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, Mwanza muda mfupi baada ya kufikishwa kutokana na kuugua ghafla. 

Kutokana na kifo cha mkurugenzi huyo, Majaliwa aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, akisitisha ziara hiyo.
 
Akizungumza mbele ya wananchi waliofika kuhani familia ya mkurugenzi huyo eneo la Uzunguni mjini Maswa jana, Majaliwa alisema amepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha ghafla cha mkurugenzi huyo.
 
Majaliwa alisema Kagenzi alikuwa mchapakazi na mwadilifu na kuwa taifa limempoteza mtumishi aliyekuwa akiendana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli kwa utendaji wake wa kazi.
 
Alisema akiwa katika ziara yake ya siku ya nne mkoani Simiyu huko wilayani Meatu, ghafla alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo, kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary Kirigini kwa njia ya simu ya kiganjani, huku akilia, alielezwa kuwa mkurugenzi huyo amefariki dunia jijini Mwanza.
 
Saa Chache kabla ya kifo chake, Kagenzi alikuwa akiendelea kuchapa kazi ofisini kwake huku akiwasiliana kwa karibu na Mkuu wa Wilaya ya Maswa kwa ajili ya taarifa ya wilaya kwa Waziri Mkuu katika siku iliyokuwa ikifuata, ambayo alikuwa atembelee huko.
 
Alisema kuwa mkurugenzi huyo ambaye alizaliwa katika kijiji cha Nyandutu, Oktoba 21, 1960 Karagwe mkoani Kagera, ameacha pengo kubwa na kuwataka familia, ndugu, jamaa,m arafiki na wananchi wa wilaya ya Maswa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
 
Akiwa katika mazoezi Ijumaa iliyopita, karibu na Shule ya Sekodari ya Wasichana ya Maswa, ghafla alijisikia nguvu zilimwishia na kukaa chini, ndipo wasamaria wema walipomfuata na kumpa huduma ya kwanza. 
 
Baada ya hapo walimpeleka katika hospitali ya wilaya ya Maswa kabla ya kumpeleka Bugando ambako aligundulika alikuwa na na tatizo la moyo.
 
Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda  Nyandutu, Karagwe kwa mazishi na msafara huo utaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Mkuu wa Wilaya ya Maswa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo