Makete inahitaji damu salama...Taarifa kamili iko hapa

Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe imesema imejipanga vilivyo kushirikiana na wananchi wa wilaya yote ya Makete kuhakikisha wanapata damu salama itakayosaidia kuokoa maisha ya wananchi wake wakiwemo wajawazito wanaokwenda kujifungua pamoja na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji

Kauli hiyo imetolewa leo na Mganga mkuu wa wilaya ya Makete Dkt Joseph Gasper Kimaro wakati akizungumza na mwandishi wetu kuhusu namna walivyojipanga kupata damu kutoka kwa wananchi wanaopenda kujitokeza kuchangia damu ili itumike katika hospitali zote za wilaya ya Makete

Amesema zoezi hilo ni la hiari ambapo mwananchi atapewa kadi kila anapojitokeza kuchangia damu, ambapo amesema baada ya kuikusanya damu kutoka kwa wananchi waliochangia wataipeleka mkoani Mbeya kwa ajili ya kuipima na kupata damu salama ambayo itarudishwa wilayani Makete tayari kwa kuanza kuitumia katika hospitali zote zilizopo wilayani hapo ambazo ni Hospitali ya wilaya ya Makete, Hospitali ya Consolatha Ikonda, Hospitali ya Bulongwa pamoja na kituo cha afya Matamba ambacho kwa hivi sasa kinatoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa

Dkt Gasper amesema kwa sasa tayari wilaya imepata kamati itakayoratibu na kufanikisha zoezi hilo ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni, na kwa sasa halmashauri imemtuma mtaalamu mmoja wa afya kwenda mkoani Mbeya kujifunza namna ya kufanikisha suala hilo na atakaporudi ataitoa elimu hiyo kwa wataalamu wengine waliosalia

"Baada ya damu zote kuchunguzwa kwa kufanyiwa vipimo vya kitaalamu, majibu yatarejeshwa hapa wilayani tayari kwa kuzitumia hivyo nawaomba wananchi wajitokeze kuchangia damu tuokoe uhai wa wote wanaohitaji kuongezewa damu katika wilaya yetu" amesema Dkt Gasper

Takwimu zinaonesha mahitaji ya damu katika wilaya nzima ya Makete kwa mwaka ni "unit" 1,344 ambapo kwa mwezi mmoja hospitali ya wilaya inahitaji Unit 10, Hospitali ya Consolatha Ikonda 90, hospitali ya Bulongwa unit 8 na kituo cha afya Matamba wanatumia unit 4


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo