Taarifa za kutozaa matunda matengenezo ya greda la halmashauri ya wilaya ya Makete zimeonekana kuwaumiza madiwani wa halmashauri hiyo hasa ukizingatia kuwa mtambo huo ni muhimu kwa uchumi na shughuli nyingi za maendeleo ya halmashauri hiyo
Akitoa taarifa za matengenezo ya greda hilo Afisa usafirishaji Bw Raphael Kalongola amesema ni kweli greda hilo lilikuwa bovu na limefanyiwa matengenezo lakini wakati likijaribiwa baada ya matengenezo hayo kumejitokeza tene tatizo jingine
Amesema kwa hivi sasa baada ya matengenezo hayo imegundulika kuwa greda hilo kwa kwenda mbele gia namba moja mpaka tatu hazifanyi kazi, na kurudi nyuma pia gia moja mpaka tatu hazifanyi kazi
Hali hiyo imeilazimu halmashauri kuwasiliana na mafundi wengine ambao wanautaalamu na tatizo la aina hiyo na wamempata fundi ambaye yupo CHIMALA mkoani Mbeya na wamemuita aje alitatue tatizo hilo na wamekubaliana Jumamosi Februari 2, 2016 afike Ikuwo lilipo greda hilo kwa ajili ya ufumbuzi wa tatizo hilo
Taarifa hiyo ilipokelewa kwa majonzi na madiwani kwa kuwa kila mmoja alitegemea kusikia kuwa limepona hali iliyomfanya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Francis Namaumbo kuwaomba wajumbe kuwa watulivu na kwamba wao kama viongozi hawalali na watahakikisha watafanya kila linalowezekana kuhakikisha greda hilo linapona
Kufuatia maelezo hayo baraza hilo limeazimia kuwa mkurugenzi na watendaji wake wafanye juu chini lifanyiwe matengenezo hayo na katika kikao cha mipango na fedha kinachotarajiwa kuketi Februari 15 mwaka huu wanategemea kupata taarifa kuwa greda hilo limepona na lipo tayari kufanya kazi mbalimbali
