Azimio la madiwani Makete kuhusu "Ambulance" za Hospitali

Katika kuonesha kujali uhai wa wananchi wake, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Makete wamemuagiza mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha hakuna kituo cha afya au zahanati yenye gari vinakosa gari kwa sababu mbalimbali ikiwemo magari hayo kufanya shughuli nyingine

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh Egnatio Mtawa na ameitoa hivi karibuni katika baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kufuatia kuibuka kwa hoja mbalimbali kutoka kwa madiwani wakilalamikia vituo vyao kukosa magari kutokana na magari ya vituo kutoonekana muda mrefu ama kupangiwa shughuli nyingine za kufanya

Diwani wa kata ya Lupila (CCM) Mh Daniel Okoka amesema ni takriban miaka miwili sasa kituo chake cha afya Lupila kimekosa gari kutokana na gari lake kuwepo katika matengenezo kwa muda mrefu na hajui hatma yake jambo lililomlazimu mwenyekiti wa halmashauri kumtaka mganga mkuu pamoja na afisa usafirishaji wilaya wajibu hoja hiyo

Mganga mkuu wa wilaya ya Makete Daktari Joseph Gasper amekiri kituo hicho kukosa gari kwa muda mrefu kutokana na gari la kituo hicho "kunoki" injini na hivyo lipo kwenye matengenezo ya kuona namna litakapotengenezwa, lakini tayari ameshateua gari lingine kutoka kwenye idara yake likafanye kazi katika kituo hicho mpaka gari husika la kituo hicho litakavyokamilika kutengenezwa

"Mh Mwenyekiti ni kweli kituo cha afya Lupila kinahitaji gari na nimeshateua gari nama STK 84 liende Lupila lakini linahitaji matengenezo madogo sana ya kawaida pamoja na kuweka tairi mpya na mchakato huo nilishauidhinisha na unaendelea kwa T.O (Afisa usafirishaji) yeye ndio anaweza kutupa majibu hapa" amesema Dkt Gasper

Akifafanua suala hilo Afisa usafirishaji katika kikao hicho amesema gari hilo linahitaji matengenezo kidogo ambapo wanaendelea nalo na pindi likimalizika siku si nyingi litapelekewa Lupila

Baada ya majibu hayo mwenyekiti wa halamashauri Mh Mtawa akatoa agizo kwa mganga mkuu wa wilaya kuwa baraza lake halitaki kusikia habari ya magari ya vituo vya kutolea huduma za afya yanabadilishiwa matumizi kwani suala hilo sio la kujadili na wala halihitaji majadala kutokana na umuhimu wa magari katika vituo hivyo hasa ukilinganisha na jiografia ya wilaya ya Makete ilivyo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo