Wachimbaji
kadhaa wamefukiwa na kifusi katika kijiji cha Sangambi wilaya ya Chunya
mkoani Mbeya, Juhudi za kuokoa uhai wao zinaendelea, taarifa tutakujuza zaidi tukuzipata.
Tinga tinga likiendelea na juhudi za uokoaji.
Watu wawili wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba madini kwenye mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo wadogo katika Kijiji cha Sang’ambi wilayani Chunya.
Watu wawili wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba madini kwenye mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo wadogo katika Kijiji cha Sang’ambi wilayani Chunya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Jeshi la Polisi (SACP), Ahamed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea
juzi majira ya saa 12:00 jioni.
Aliwataja watu ambao wanaohifiwa kufa kwa kufunikwa na kifusi ndani
ya mgodi huo kuwa ni Christopher Wambura ambaye alikuwa akiishi
kijijini hapo lakini akiwa ni mwenyeji wa Musoma mkoani Mara na Riziki
Simkoko mkazi wa Mbozi.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Msangi alisema kuwa aliyebaini
kuwapo kwa watu waliofukiwa na kifusi ndani ya mgodi huo ni binti mmoja
ambaye hajafahamika aliyekuwa akienda kwenye kambi la wachimbaji hao
wadogo kwa ajili ya kuomba shoka.
Alisema binti huyo alipofika kwenye kambi hiyo hakuwakuta
wachimbaji hao, lakini akaona kamba mbili zilizokuwa zimeingia kwenye
shimo la mgodi uliopo karibu na kambi hiyo huku kukiwa na udongo
ulioonekana umeporomoka.
Kamanda Msangi, alisema binti huyo aliamua kuwaita wachimbaji hao
kwa sauti na ndipo aliposikia sauti za watu zikiitika kutokea ndani ya
shimo ambalo limeporomoka.
“Kusikia hivyo ndipo msichana huyo akapiga kelele na watu
wakakusanyika na kuanza jitihada za kuwaopoa ndani ya shimo hilo la
mgodi,” alisema Kamanda Msangi.
Hata hivyo, alisema wakati wananchi wakijaribu kuwaokoa watu
waliofunikwa kwenye kifusi, udongo mwingine uliporomoka na kutaka
kufukia watu wengine, huku baadhi ya waokoaji hao pia wakijeruhiwa.
Kamanda Msangi alisema wananchi hao baada ya kuona hivyo
walisitisha zoezi la kuwaokoa watu hao na ndipo walipopiga simu kwa Mkuu
wa Wilaya ya Chunya, Elias Tarimo, kwa ajili ya kuomba msaada.
Alisema mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya, akishirikiana na kamati yake
walielekea kijijini hapo huku pia wakipeleka tingatinga kwa ajili ya
kusaidia shughuli ya uokoaji.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, hadi jana jioni watu hao walikuwa
bado hawajaopolewa ndani ya shimo la mgodi na kwamba shughuli za kufukua
kifusi kwa ajili ya kuwaokoa zilikuwa bado zikiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya mkoani hapa, Abbas Kandoro jana alitembelea kijijini hapo
na kushuhudia shughuli za uokoaji zikiendelea.
Akizungumza na wananchi kijijini hapo, Kandoro aliwaonya wachimbaji
wadogo wadogo kutoendelea kuchimba kwenye migodi hiyo kwa kutumia zana
duni katika kipindi cha mvua kwa madai kuwa wanahatarisha maisha yao.