Zikiwa zimepita siku nne tangu aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo kuzikwa kijijini
kwake Chikobe, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum
Mwalimu amesema wamelazimika kuitorosha familia yake ili
kunusuru maisha yao baada ya watu wasiojulikana kuvamia
nyumbani kwake, kufanya fujo na kujaribu kuvuruga kaburi
lake kwa kutawanya udongo.
Mwalimu alisema jana kuwa wamelazimika kuitosha familia
hiyo na kupelekea kuishi mahali ambako wana uhakika kuwa ni
salama kwa maisha yao.
Alisema watu hao baada ya watu hao kushindwa kuliharibu,
waling’oa bendera za Chadema zilizokuwa zikipepea kwenye
kaburi hilo na nyingine kwenye Jimbo la Busanda, huku wakiwapiga wafuasi wa chama hicho,
akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa huo, Husna Amred na kumjeruhi
mwilini.
Mwalimu alisema wakati Rais John Magufuli akifungua Bunge mjini Dodoma hivi karibuni
aliwahakikishia Watanzania kuwa ataongoza nchini bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, lakini
yanayotokea mkoani Geita ni mambo ya kusikitisha na kutishia usalama wa maisha ya baadhi ya
watu.
Alidai kuwa kuna ya makundi ya vijana yanazunguka mitaani na kushambulia vijana wa Chadema
ambao wanapaswa kukemewa kwa nguvu zote ili kulinda amani na utulivu.
“Vitendo vinavyoendelea kutokea viongozi wa Chadema na wafuasi wao tunaelekea kuchoka
kupigwa, kuuawa, kunyanyaswa na kunyimwa haki zetu … muda unakaribia sisi kunyanyuka
endapo havitakomeshwa.
Kamanda wa polisi mkoani Geita na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest
Mangu wasipuzie yanayoendelea kutokea kwani hayawezi kuvumilika na ni kinyume na sheria,”
alionya Mwalimu.
Polisi: Hatuna taarifa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli alisema hana taarifa za kutokea kwa fujo
hizo nyumbani kwa marehemu Mawazo kijijini hapo wala kujeruhiwa kwa mtu yeyote na kuahidi
kufuatilia kisha kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.
