FAMILIA ya Leticia Nyerere, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema)
katika Bunge lililopita, itatoa tamko kuhusu hali ya afya ya mwanasiasa
huyo Ijumaa wiki hii, baada ya kupata taarifa ya madaktari
wanaomtibu.
John Shibuda ambaye ndiye msemaji wa familia, alisema jana
kwamba kinachoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mbunge huyo wa
zamani amefariki dunia ni uzushi, kwa kuwa mgonjwa bado anaendelea
kupata tiba kutoka kwa madaktari wake.
“Ninachoweza kukwambia ni kwamba kama familia tutatoa tamko rasmi Ijumaa kuhusu afya ya dada yetu na tutazungumza baada ya kupata taarifa za kina ya madaktari wanaomtibu,” alisema Shibuda.
Shibuda alisema kwa sasa hawana cha kuzungumza bali
wanachojua ni kwamba ndugu yao bado anapata matibabu huko Marekani;
“Tumeongea na madaktari watatupa taarifa zaidi Ijumaa na sisi hapo ndipo
tutakapotoa taarifa kwa umma.”