JESHI la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mkazi wa Lamadi, Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, Grace Ndimishinji (36), kwa tuhuma za kukutwa akijihusisha na ushirikina katika Kijiji cha Lamadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gemini Mushy, alisema tukio hilo ni la kipekee kutokea katika Mkoa huo ambapo mtuhumiwa alikutwa uchi wa mnyama asubuhi kwenye familia ya Yusta Thomas (35).
Alisema mtuhumiwa alikutwa jikoni Desemba 22, mwaka huu akiwa amening'inia bila kujitambua ambapo mama mwenye nyumba baada ya kumuona, alipiga kelele akiomba msaada kwa majirani," alisema.
"Siku ya tukio, mume wa Yusta ambaye ni mfanyabiashara wa samaki
hakulala nyumbani... alipofika nyumbani alilikuta tukio hilo, alimwamuru
mama huyo ashuke chini alikokuwa amening'inia akiwa uchi, wakati huo
polisi walifika eneo hilo, kumvisha nguo, kwenda naye kituoni. Mtuhumiwa
anaendelea kufanyiwa uchunguzi ambao ukikamilika, atafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma za ushirikina," alisema.
Kwa upande wake, Yusta alisema saa nane usiku, alisikia sauti za watu
wakiitana majina bila kuwajua akina nani lakini wakati huo mbwa wao
alipobweka, watu hao waliacha mazungumzo na kunyamaza.
"Mwanangu wa kike aliniambia kuna watu wanazungumza nje ya nyumba na
walipoamka asubuhi walimkuta mtuhumiwa akining'inia jikoni na kuomba
asamehewe akidai dereva wake amemwambia ashuke pale atampitia.
"Mtuhumiwa alikuwa amebeba kiberiti kisichokuwa na njiti, majaribu ya
kimiujuza yamekuwa yakijitokeza katika nyumba yetu mara kwa mara lakini
tukio hilo liliwashangaza sana," alisema.
Alipoulizwa ni vitu gani vilivyochangia mama huyo anase nyumbani
kwake na utaalamu gani waliotumia kumshusha, Yusta alidai ni maombi
pekee kwani tangu alipoanza kusikia minong'ono nje alianza kuomba.