Serikali imeombwa kuiokoa Shule ya Msingi Ilembo katika kijiji cha
Ilembo Mbeya Vijijini kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uchakavu wa
majengo, ukosefu wa madawati, nyumba za walimu na uchache wa Walimu.
Wakazi wa kijiji cha Ilembo wamesema hali hiyo imesababisha watoto
wao kutopata elimu wanayostahili na hivyo kufanya vibaya kwenye mitihani
ya kumaliza elimu ya msingi.
Shule ya Msingi Ilembo, iliyopo katika kijiji cha
Ilembo, Mbeya Vijijini, imejengwa mwaka 1954 na katika uhai wake wa
miaka 61 imefanikiwa kutoa elimu kwa wakazi lukuki wa kijiji hicho ambao
kwa sasa wanaendesha maisha sehemu mbalimbali mkoani Mbeya na mikoa
mingine ya Tanzania.
Shule hii kwa sasa ipo dhoofulhali, ubovu wa madarasa, uchakavu wa
madawati na uhaba wa walimu ni changamoto zinazoelezwa na wakazi wa
Ilembo kuwa ni kikwazo katika utoaji wa elimu bora kwa watoto wao.
Malalamiko ya wananchi hao yanaungwa mkono na
Mwenyekiti wa kijiji hocho, Anthony Ndege ambaye anasema kuwa serikali
inapaswa kuharakisha ili kutatua changamoto hiyo kwani shule hiyo
inategemewa na wananchi wengi wa kijiji hicho.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Juma Kenani, amesema angalau wameanza mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Changamoto hizo zinawasukuma baadhi ya wananchi waliosoma kwenye
shule hiyo miaka kadhaa iliyopita kuitumia sikukuu ya Chrismas kutoa
msaada wa madawati shuleni hapo kupitia Umoja wao unaojulikana kama
Ilembo Family.
Shule ya Msingi Ilembo, ni miongoni mwa shule zilizopo maeneo ya
vijijini ambazo zinahitaji juhudi za makusudi za wadau wa elimu na
wananchi kwa ujumla ili kuziokoa na hali mbaya inazozikabili.