
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo
ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo, CHADEMA, kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Abraham
Mwanyamaki, dhidi ya Mbunge wa Kyela na Waziri wa Katiba na Sheria,
Dokta Harrison Mwakyembe.
Mahakama imefikia hatua hiyo baada ya Mwanyamaki kushindwa kulipa ada
ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo shilingi Milioni Tatu katika muda
wa Siku 14 uliowekwa kisheria.
Baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015, Jumla ya kesi Sita
zimefunguliwa kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, kupinga matokeo ya
uchaguzi, Tano ni za waliokuwa wagombea wa CHADEMA dhidi ya walioshinda
kutoka CCM na Moja ni ya Mgombea wa CCM dhidi ya aliyeshinda kwa
CHADEMA.
Hata hivyo, Jaji wa mahakama hiyo, Atuganile Ngwala, ameitupilia
mbali kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea wa CHADEMA, katika jimbo
la Kyela, Abraham Mwanyamaki, dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa
Katiba na Sheria, Dokta Harrison Mwakyembe, baada ya Mwanyamaki
kushindwa kulipa ada ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo ambazo ni
shilingi Milioni Tatu katika muda uliowekwa wa siku 14 kuanzia Disemba
10 hadi 23 mwaka huu.
Mbali na kuifuta kesi hiyo, Jaji Ngwala, pia amemuagiza Mwanyamaki,
kulipa gharama zilizojitokeza kwa upande wa Mlalamikiwa Dokta Mwakyembe
na jopo la Wanasheria wake kutokana na matumizi waliyoyafanya katika
kufuatilia shauri hilo hadi linatupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Licha ya kulifuta shauri hilo, mahakama hiyo imeridhika kuwa kesi
nyingine Tano zimekidhi vigezo vya kisheria hivyo zitatajwa mahakamani
hapo Januari Saba mwakani ili kuendelea na taratibu za kisheria za
uendeshaji wa kesi za aina hiyo.
Kesi hizo ni iliyofunguliwa na Kada wa CCM Dokta Lucas Siyame dhidi
ya Mbunge wa Momba kupitia CHADEMA, David Silinde, kesi ya John
Mwambigija wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa Rungwe kwa tiketi ya CCM, Saul
Amon na shauri la Liberatus Mwang’ombe wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa
Mbarali, Haroun PirMohammed wa CCM.
Kesi nyingine ni ya Fanuel Mkisi wa CHADEMA akipinga ushindi wa
Mbunge wa Vwawa kupitia CCM, Japhet Hasunga na shuari lililofunguliwa na
Adam Zela wa CHADEMA dhidi ya Mbunge wa Mbeya Vijijini kwa tiketi ya
CCM, Oran Njeza.
Mbeya ina majimbo 13 ya uchaguzi, kutokana na kesi hizo Wabunge wa
majimbo Manane ambayo ni Mbeya Mjini, Lupa, Songwe, Tunduma, Mbozi,
Ileje, Busokelo na Kyela ndiyo wenye uhakika wa kuendelea na shughuli
zao za ubunge bila ya kutikiswa na kesi mahakamani.