Mkazi wa kijiji cha Msasa kata ya Busanda wilayani Geita Lucas Perto anashikiliwa kwenye ofisi ya Afisa mtendaji wa kata hiyo kwa tuhuma ya kuwaunguza midomo, mikono na miguu watoto wake akiwatuhumu kuiba mboga aina ya samaki kwa jirani yake.
Baada ya kutekeleza ukatili huo Desemba 6 mtuhumiwa mwenye umri wa miaka 29 aliwaficha watoto wake hadi Desemba 12 walipogunduliwa na wasamaria wema wakiwa wameanza kutoa harufu mbaya.
Wahudumu wa Afya ya msingi ya jamii ndiyo waliookoa maisha ya watoto wakati wakikagua zoezi la utekelezaji usafi wa mazingira baada ya kudokezwa na wasamaria wema.
Watoto hawa wawili Denis Lucas mwenye umri wa miaka saba (7) na Esther Lucas miaka mitano (5) walikuwa wamefichwa ndani wakiwa na hali mbaya baada ya kuunguzwa kwa moto na Baba yao mzazi.
mtendaji wa kata ya Busanda Justa Mabara afisa amesema amesikitishwa na kitendo hicho cha kikatili na hivyo kuahidi sheria kuchukua mkondo wake.
Kwa upande wake Baba mzazi wa watoto hawa amekiri kutekeleza ukatili huo na kudai Lucas amesema watoto wake wanalelewa na mama wa kambo baada ya mama yao mzazi kutalikiana naye.
Hata hivyo watoto hawa wawili wamehamishwa kutoka zahanati ya Busanda ambapo walikuwa wamelazwa na kuhamishiwa katika hospitali ya wilaya baada ya hali zao kuzidi kudhoofika.
