Waomba Magufuli awalinde baada ya kumkamata muuguzi kwa "kuiba dawa za kituo cha afya"

Katika hali hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wakazi wa kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga wamefanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga katika kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga akituhumiwa kuiba dawa za kituo hicho.


Mashuhuda wa tukio hilo la aina yake wameiambia blog hii kuwa limetokea jana majira ya saa tano asubuhi katika eneo la kituo cha afya Kambarage Shinyanga baada ya wananchi takribani saba kumtilia shaka muuguzi huyo aliyejulikana kwa jina la Joseph Nkila waliyemuona akitoka kituoni hapo akiwa ameficha mfuko waliohisi kuwa ni dawa za serikali. 

Muuguzi amekamatwa na wananchi akiwa na kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin Syrup. 

Wakisimulia jinsi walivyomkamata, Rashid Shaban na Kagoma Hamis kati ya wananchi saba wanaofanya shughuli zao karibu na kituo hicho cha afya wameiambia blog hii kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikerwa na mchezo mchafu wa muuguzi huyo ambaye mara nyingi amekuwa akionekana na maboksi ya dawa yenye nembo ya MSD na mara nyingi amekuwa akiegesha gari lake kwenye eneo lao la kazi na kisha kupakia dawa hizo kwenye gari jingine na ndipo jana walipoamua kuchukua hatua. 

Wamesema jana kama kawaida yake alifika eneo hilo na kisha kushusha mfuko na kuuweka kwenye gari jingine na kumpa maelekezo dereva wa gari hilo na kuondoka haraka kutoka eneo hilo na kumuacha dereva wa gari hilo la pili, ndipo walipoamua kuzuia gari hilo na kumbana dereva aliyewaonesha dawa na kudai kuwa huwa wanazisafirisha kwenda kijijini.

Hamis aliiomba serikali kuwahakikishia usalama wa maisha yao kwani sasa wanapata vitisho baada ya kufichuo uovu huo. Amesema kutokana na uwepo wa serikali makini ya rais Magufuli, wameamua kujitoa muhanga ili kuokoa jamii kwa kuamini kuwa serikali itawahakikishia usalama wao.


Kaimu Mganga Mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael amesema ni kweli muuguzi huyo amekamatwa na dawa hizo ambazo hazina nembo ya MSD ingawa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ni dawa za kituo hicho.

‘Sisi kama uongozi wa Mkoa na Halmashauri kwenye usimamizi wa dawa hatufanyi utani. Tunaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake kwa maana ya kuchunguza ili kubaini ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe,”ameongeza Dkt Raphael. 

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amethibitisha kukamatwa kwa muuguzi huyo na kusema bado wanaendelea kumhoji juu ya hilo. 
  • Imeandikwa na Kadama Malunde via Malunde1 blog


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo