Rais Magufuli: Hakuna sherehe ya Uhuru mwaka huu, Badala yake mkafanye Usafi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA, 
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kwa mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi. Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.

Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.

Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23 Novemba, 2015


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo