Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limezuia maandamano ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) yaliyopangwa kufanyika leo Novemba 03,2015 katika mji wa Shinyanga kwa lengo la kupinga matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,2015.
Akizungumza na waandishi wa habarijana, kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alisema wamezuia maandamano yaliyopangwa na Chadema kufanyika Novemba 03,2015 akidai kuwa katika kipindi hiki hawaruhusu kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa sababu jeshi la polisi limejikita katika kuangalia hali ya usalama ili kusubiria kuapishwa kwa rais mteule na wabunge.
Alisema pia wamezuia mikusanyiko yoyote isiyo rasmi ambayo inaweza kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Kamugisha alisema Chadema walitoa taarifa kuwa leowanataka kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25,2015 na baada ya kufanya maandamaano hayo wanataka kutoa ujumbe kwa serikali.
Aliwashauri wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga wasishawishiwe na viongozi wa vyama vya siasa,na kuwaomba wabaki majumbani,waendelee na shughuli zao na kutokubali kurubuniwa au kushawishiwa kuandamana kwani wanaowashawishi hawatakuwa mbele .
Katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga mjini George Kitalamaalisema hawajapata taarifa wala maelekezo yoyote kuhusu kuzuiwa kwa maandamano yao na wanaendelea kujiandaa na wanachama wao kwa maandamano kama walivyopewa maagizo na viongozi wao wa kitaifa.
Alisema leo tarehe 03.11.2015,watafanya maandamano ya amani kuanzia ofisi za Chadema wilaya kisha kuzunguka mji mzima wa Shinyanga kuanzia saa tatu asubuhi kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume,na kwamba ni maandamano ya nchi nzima siyo Shinyanga pekee.