JESHI la polisi Mkoani Singida limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa na vyama vya siasa vilivyosimamisha mgombea wa Urais chini ya mwavuli wa UKAWA,kufanyika nov,03,mwaka huu kwa nchi nzima kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya uchaguzi nchini (NEC).
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake jana,kamanda wa polisi Mkoa wa Singida,Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Thobias Sedoyeka , alisema pamoja na kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa,vyama hivyo vinaitaka pia mamlaka husika kumtangaza mgombea wao katika Uchaguzi,Bwana Edward Lowasa wakiamini kuwa ndiye mshindi wa kiti cha Urais.
AIDHA Kamishna Msaidizi wa polisi huyo alifafanua kwamba uchunguzi unaonyesha kuwa maanadamano hayo yatashirikisha makundi mbalimbali ya watu,hususani vijana zaidi na kupita sehemu mbalimbali za Mji kabla ya kuhitimisha katika Ofisi walizolenga.
KWA upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) Mkoa wa Singida,Bwana Shabani Limu amekiri kupokea maagizo kutoka ngazi za juu za chama hicho,na kuongeza kuwa mpaka sasa bado hakuna mafanikio ya kufanyika kwa maandamano hayo kutokana na makamanda wa polisi wa wilaya zote kutoyaruhusu kwa kuhofia uvunjifu wa amani.