Kipindupindu chaitikisa Dodoma

Maji yasiyo salama ni moja ya chanzo cha ugonjwa wa kipindupindu.

JUMLA ya watu 87 katika wilaya ya Bahi katika Mkoa wa Dodoma wamegundulika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu.

Hayo yalielezwa na Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Bahi, Dk. Gerald Maro alipokuwa akizungumza na MwanaHALISI Online juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu katika wilaya hiyo.
Dk. Maro amesema mgonjwa wa kwanza aligundulika Oktoba 21 mwaka huu ambaye alitokea kata ya Mpamatwa ambapo wagonjwa wengine waliendelea kujitokea hadi kufikia 81 hadi sasa.
Hata hivyo amesema wagonjwa wengine sita wa kipindupindu walitokea kata ya Bahi Makulu na kata ya Mtitaa na kufanya wagonjwa wote kufikia 87 hadi leo.
Akitoa ufafanuzi amesema hadi jana wagonjwa watatu ndiyo pekee wamelazwa katika kambi maalum ya kuwashughulikia wagonjwa hao huku wagonjwa wa kipindupindu 84 wakiwa wameruhusiwa na kurudi majumbani kwao.
Akizungumzia suala ya kujitokeza kwa maambukizi hayo amesema ni kutokana na kuwepo kwa tatizo la maji yasiyo safi na salama.
“Hapa Bahi kuna tatizo kubwa la uhaba wa maji safi na salama kutokana na hali hiyo watu wanatumia maji ya kisima vifupi ambavyo kimsingi maji yake si salama sana.
“Hata hivyo kutokana na hali ya kuzuka kwa kipindupindu uongozi umefanya kila jitihada za kuhakikisha maji yanatibiwa na kwa sasa visima vyote vya maji vimewekewa dawa ya kutibu maji,” amesema Dk. Maro.
Jambo lingine lililochangia mlipo wa ugonjwa huo, amesema ni tatizo kubwa la kaya nyingi kutokuwa na vyoo bora jambo ambalo linaweza kusababisha kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa kama hayo.
Dk. Maro amesema kwa sasa wananchi wanapatiwa elimu ya kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama ikiwa ni pamoja na kuwa na vyoo ambavyo ni bora kwa lengo la kujiepusha na mlipuko wa magonjwa kama hayo.
Mbali na hilo amesema viongozi wa kata mbalimbali ambao wanatoka wagonjwa wanaimizwa kutoa elimu kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuimiza swala la usafi ili kuifanya jamii kuwa katika mazingira ambayo ni salama zaidi.
Katika mkoa wa Dodoma kwa sasa watu wawili kutoka kata ya Mkoka wilayani Kongwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo