Mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Dokta Thomas Rutachunzibwa amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu wawili kutokana na ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo.
Aidha Mganga huyo amesema hadi hivi sasa jumla ya wagonjwa kumi na wawili waliokutwa na vimelea vya ugonjwa huo,wanaendelea na matibabu katika kambi maalum iliyopo katika hospitali ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa kutapika na kuharisha na kuthibitika kuwa si kipindupindu sasa imebainika wazi kuwa wagonjwa wawili wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
kwa mujibu wa Star TV iliwatembelea wagonjwa wengine kumi na wawili wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Manispaa ya Bukoba iliyopo eneo la Nshambya ,ambao wanaendelea vizuri na matibabu.
Mganga mfawidhi wa kituo hicho cha Nshambya ,Felista Rweyemamu amesema hali za wagonjwa hao zinaendelea kuimarika kutokana na kuwa katika hali ya uangalizi wa madaktari.
Kadhalika Idara ya Afya mkoani Kagera , imeendelea kutoa tahadhari kwa wakazi wa mkoa huo,kufuata kanuni za afya ya msingi na kusaidia kutoa taarifa kwa mtu yeyote anayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo,ili aweze kupatiwa matibabu ya haraka.