Viongozi wa Dini nchini wametakiwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi wakati wanapotaka kusajili taasisi zao kwa ajili ya kutoa huduma za kiroho.
Tamko hilo limetolewa kwa madai kuwa baadhi ya Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste ambao hawako kwenye Baraza la Makanisa nchini wanakiuka taratibu za usajilli.
Maaskofu hao wamelilaumu Baraza la Makanisa ya Kipentekoste na Serikali kuwa wanazuia usajili kukiwa na tetesi ya kutaka kufutwa kwa baadhi ya taasisi.
Akijibu malalamiko hayo katika mkutano wa viongozi wa dini jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania David Mwasota anasema ni lazima taratibu zifuatwe.
Katika Mkutano huo pia kuliibua suala la viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuvipigia kampeni vyama vya siasa.
Sambamba na hilo pia wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuondoa majina ya viongozi wote wa dini watakaoshiriki kusimamia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba.
Wamesema iwapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitachukua hatua ya kuwaondoa viongozi wa dini kusimamia uchaguzi, kauli za kuwakataza viongozi hao kujiingiza kwenye siasa hazitakuwa na maana.