Serikali na asasi zinazojishughulisha kutoa elimu ya uraia kuhusu masuala ya upigaji kura wametakiwa kuyafikia makundi ya wanafunzi wa sekondari waliofikisha umri wa kupiga kura pamoja na wakazi walio maeneo ya vijijini ili waweze kupiga kura kwa usahihi.
Elimu hiyo inahusu namna ya kuzingatia taratibu ndani ya chumba cha kupigia kura ikiwa na nia ya kuzuia uharibifu wa kura unaoweza kutokea kwa kukosa elimu ya namna hiyo.
Wakizungumza wakati wakitoa elimu ya jinsi ya kupiga kura katika shule ya sekondari ya Arusha iliyopo jijini hapa wahamasishaji kutoka asasi inayojishughulisha na vijana ya TYVA wamesema kundi la vijana walio shuleni hawapati muda wa kutosha kufuatilia yanayojiri katika harakati za uchaguzi ukilinganisha na vijana walio mitaaani.
Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya sekondari ya Arusha wamesema wanafunzi hawana utaratibu mzuri wa kushiriki nyakati za uchaguzi na pia wamependekeza somo la elimu ya uraia litiliwe mkazo kwa kipindi ambacho wapo shuleni.
Wananchi wanatakiwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na tume ya Taifa ya uchaguzi ili kufanikisha zoezi la upigaji kura litakalofanyika jumapili ya octoba ishirini na tano.