Wakati joto la uchaguzi likizidi kupanda
nchini, wagombea wa urais wanatarajiwa kuchuana vikali
kunadi sera zao kwa wananchi katika mdahalo utakaofanyika
Oktoba 18 jijini hapa.
Vigogo hao watakuwa na kibarua cha kujibu maswali
mbalimbali kutoka kwa wananchi na kueleza kinagaubaga sera
namna watakavyozitekeleza iwapo watachaguliwa.
Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze amewaambia
waandishi wa habari leo kuwa mdahalo huo utahusisha wagombea kutoka katika vyama vya
Alliance for Democratic Change (ADC) ACT-Wazalendo, Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa,
Chaumma na CCM.
Amesema wamevialika vyama hivyo kutokana na kusimamisha wagombea wa urais katika jamhuri
ya muungano na visiwani Zanzibar na kuwa na wagombea wa ubunge wasiopungua 55.
Hata hivyo, amesema hadi leo ni vyama vitatu tu vya ADC, ACTWazalendo na Chaumma pekee
ndivyo vilivyokubali kushiriki huku CCM na Chadema vikiwa bado havijathibitisha ushiriki huo.
“Tunaendelea kuwashawishi wagombea wa vyama vilivyobaki ili ushiriki wao kwenye tukio hili la
kihistoria. Tumetuma barua rasmi kwa vyama vyote na tunafuatilia ili wathibitishe ushiriki wao
mapema iwezekanavyo,” amesema Eyakuze.
Mapema mwezi uliopita CCM kilitangaza kuwa mgombea wake wa urais Dk John Magufuli
angeshiriki mdahalo huo huku Ukawa kupitia Mwenyekiti mwenza, James Mbatia wa NCCRMageuzi,
ulisema wanahitaji mdahalo wa viongozi wa vyama na siyo wagombea.
Eyakuze amesema mdahalo huo umeandaliwa chini ya muungano wa taasisi mbalimbali za CEE
Roundtable, Tanzania Media Foundation (TMF), Twaweza na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake (Tamwa).
Alipoulizwa iwapo watakubali pendekezo la kupokea viongozi wa vyama badala ya wagombea,
Eyakuze amesema waandaji hao hawatabadilisha mfumo walioupanga na kwamba mdahalo
utafanywa na wagombea watakaojitokeza.
“Sisi tunataka wagombea husika waliothibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hatubadilisha
mfumo tuliojiwekea hata kidogo. Hatujakata tamaa bado tunaendelea kuwashawishi washiriki ili
wananchi waweza kuwasikiliza’’, amesema Eyakuze.