Mwenyekiti wa CUF na wengine 15 mbaroni kwa tuhuma za kuchoma makanisa Bukoba

Jeshi la Polisi limewakamata watu 16 akiwamo Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Bukoba kwa madai ya kuhusika na vitendo vya uchomaji wa makanisa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bukoba. 

Watu hao, wakiwamo viongozi na wanachama wa CUF, walikamatwa juzi na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Kagera na Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Augustine Ollomi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa atalitolea ufafanuzi suala hilo leo. 

Waliokamatwa katika tukio hilo, ni diwani aliyemaliza muda wake Kata ya Katoro (CUF), Amini Mashaka, Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Bukoba Vijijini, Ladslaus Kashonda, Rwegasira Kashonda, Abdul Dauda, Mwalimu Shakuru Katakweba, Sulaiti Katima, Mudathiru Rukindo, Hashimu Kanyonyi, Abdul Nkingireha, Sadiq Mustafa, Hassan Bakuza, Suleiman Mfuruki na mwingine aliyetambulika kwa jina la Jasson. 

Mgombea ubunge wa CUF, Jimbo la Bukoba Vijijini, Buberwa Kaiza alidai kuwa wote waliokamatwa ni viongozi wa chama hicho na wamebambikizwa tuhuma za kuchoma makanisa na kukamatwa usiku wa kuamukia leo. 

Kaiza alisema kwa mtu anayejua mwelekeo wa kampeni za ubunge na udiwani katika kata za Katoro, Nyakibimbili, Kasharu, Kaibanja na Kishogo atakuwa anafahamu kuwa masuala hayo yanahusiana na masuala ya kampeni Hofu ya wananchi Wakazi wa Kata za Katoro na Kaibanja ambako yalitokea matukio matatu ya uchomaji wa makanisa usiku wa kuamkia Jumapili, walisema suala hilo limeleta hofu zaidi kwa kuwa hata kundi lililokuwa linacharaza wananchi na kuharibu mali kabla ya hapo halikuwahi kujulikana, huku wengine wakisema ni la kisiasa. 

Pamoja na matukio ya uchomaji kutokea katika Kata ya Kaibanja, watuhumiwa zaidi ya 15 waliokamatwa wakihusishwa na matukio hayo wote wanatoka kata jirani ya Katoro. 

Baadhi ya wananchi wameshangaa kukamatwa kwa mgombea udiwani wa Katoro, Mashaka akihusishwa na uchomaji wa makanisa wakati amewaongoza kwa vipindi viwili mfululizo sasa. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kaibanja, Muganyizi Bagandanshwa alihusisha vitendo vya uchomaji wa makanisa na kuibuka upya kwa kundi la ‘wakacharaji’. Bagandanshwa alisema vitu vilivyoteketezwa ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Mtaa wa Kaibanja vina thamani ya zaidi ya Sh2 milioni na vilikusanywa eneo anaposimama kiongozi wa ibada kabla ya kuteketezwa. 

Mchungaji wa Kanisa la Faith Mission lililopo katika Kijiji cha Kaibanja, Laurent Komba alisema yeye na waumini wake wanaishi kwa hofu wakiamini matukio yaliyotokea kwenye makanisa jirani yanaweza kuwafikia pia.

Chanzo:Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo