Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi,
Mwanaspoti na The Citizen, imelaani vikali upotoshaji wa
makusudi unaolenga kutumia jina la Mwananchi kuwachafua
wanasiasa na watu wengine hasa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi
Mkuu.
Mapema wiki hii, watu wasio na nia njema walitengeneza mfano
wa gazeti la Mwananchi kwenye mitandao ya kijamii likionyesha
habari ya kumchafua Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi,
ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa umoja wa
vyama vinavyounda Ukawa, James Mbatia.
Mhariri Mtendaji
Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alishauri timu za kampeni za
vyama vyote, kunadi sera zao na kuonyesha jinsi watakavyozitimiza badala ya kusambaza
propaganda zinazolenga kuchafua jina la kampuni ya Mwananchi.
Alisema MCL inapanga
kuwasilisha malalamiko rasmi kwa vyombo vya sheria ili vichukue hatua kutokana na udhalilishaji
huo.
Hii si mara ya kwanza kwa watu wenye nia mbaya na magazeti ya kampuni ya Mwananchi
kutengeneza mfano wa gazeti na kuandika vichwa vya habari ambavyo vina lengo la kuichafua.
Machumu alisema ingawa MCL haihusiki kwa vyovyote vile na gazeti feki hilo lililokuwa
linasambaa kwenye mitandao, inamuomba radhi Mbatia na wengine wote walioumizwa na
kitendo hicho.
