Ombi la Chadema la kutaka wataalamu wa
Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa
waruhusiwe kukagua programu itakayotumika kuhesabu kura
za urais, limesababisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kukitaja chama hicho kuwa ndicho pekee kinachoipa shida
katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji
mstaafu, Damian Lubuva ambaye hata hivyo alisema Tume
yake itakutana na wawakilishi wa vyama vyote muda mfupi
kabla ya siku ya upigaji kura ili watoe madukuduku
waliyonayo.
“Tunasubiri walete hilo ombi. Lakini hata wasipofanya hivyo tutakuwa na kikao na vyama vyote
vya siasa baada ya kumalizana na wadau wengine.
“Chadema wana wasiwasi mwingi na ndicho chama kinachotupa shida mara nyingi.
Tukifanya
hivi, wao wanataka hivi,” alisema Jaji Lubuva alipokuwa akijibu maombi ya Chadema
yaliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wake, John Mnyika alipozungumza na vyombo vya
habari.
Mnyika aliitaka NEC kuruhusu wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa
kimataifa nao waende NEC na wataalamu wao kuhakiki mfumo utakaotumika kupokelea kura
za urais kwa lengo la kujua kama uko salama ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Mnyika alidai kuwa kuna mazingira ya kupigwa ‘bao la mkono’ yanayotengenezwa na ndiyo
maana ni muhimu mambo yote yakawekwa wazi ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
“Lubuva akubali kuanzia sasa tuchambue huo mfumo na wataalamu wetu waukague ili wajue
kama uko salama usije ukawa ni wa kuiba kura na kutupiga ‘bao la mkono’,” alisema Mnyika.
Mbali na hilo, Mnyika alidai kuwa anashangaa kwa nini NEC hadi sasa haijawasilisha daftari la
awali la wapigakura kwa vyama vya siasa ili walihakiki.
“Kwa nini hadi sasa hawajatukabidhi daftari, lazima tupewe kama ilivyofanyika mwaka 2010,”
alisema Mnyika na kuongeza: “Suala la kwamba NEC inasema uhakiki umefungwa wakati sisi
hatujakabidhiwa hilo daftari kulihakiki, kuna mazingira ya bao la mapema la mkono.”Mnyika alisema mwaka 2010, daftari hilo lilivisaidia vyama vya siasa kuwaonyesha wananchi
ambao walikosa majina yao vituoni kuwaelekeza vituo vyao kutokana na majina kuwapo
kwenye daftari lakini yakikosekana kwenye orodha zinazobandikwa vituoni.
“Daftari hili ni muhimu sana, mwaka 2010 tuliweka dawati letu kwenye vituo.
Wananchi ambao
walifika kituoni na kukosa majina yao kwenye orodha iliyobandikwa tuliwaambia waende
kwenye dawati la Chadema waangaliziwe kwenye daftari na walipokuta majina yapo
tuliwaambia wapige kura na walifanya hivyo bila matatizo,” alisema Mnyika.
Aliwataka wananchi kuwa makini na suala hilo na kuhakikisha wanapiga na kulinda kura ili
kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Pamoja na kwamba Jaji Lubuva alisema matokeo yote yatabandikwa vituoni, hivyo wananchi
wapige kura na kuondoka, Mnyika alipinga na kuwataka wananchi kutomsikiliza kwani
kuondoka vituoni kunatoa mazingira ya kuibwa kura.
Hata hivyo, Mnyika alisema pamoja na mazingira mbalimbali ya bao la mkono
yanayotengenezwa, mwaka huu ni wa mabadiliko, hivyo wana Ukawa wasikate tamaa.
