Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia mgombea ubunge jimbo la Solwa kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Jeremiah Msandete kwa kosa la kukamatwa na mapanga,nondo,makombeo na mawe yanayodaiwa kutumika wakati na baada ya uchaguzi kushambulia wananchi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,JANA jioni,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alisema silaha hizo zimekamatwa kwa awamu mbili ambazo ni vipande vya nondo 146,makombeo 20,mapanga 12,viroba vya pombe pakti 264 na mawe 10.
Alisema tukio la kwanza limetokea Oktoba 24,2015 saa nne usiku katika eneo la Lubaga wilaya ya Shinyanga askari polisi walikamata gari lenye namba za usajili T.110 AVR Toyota Sprinter mali ya Jeremia Mshandete(39) mkazi wa Nyegezi mkoani Mwanza ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Solwa kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kamanda Kamugisha alisema gari hiyo ilikuwa imebeba bendera moja ya CCM iliyochanwa,vipande vya nondo 138,kombeo 17,pombe aina ya Vodka pakti 120 na Valeur pakti 144 na mapanga matatu.
Alisema gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Mfati Jackson(27) na ndani ya gari alikuwemo abiria aitwaye Ngasa Salaganda na wote wanashikiliwa na jeshi la polisi.
Kamanda Kamugisha alisema awamu ya pili ya ukamataji wa silaha ilikuwa Oktoba 25,2015 saa tatu usiku katika maeneo ya Bushoma wilaya ya Shinyanga ilikamatwa gari lenye namba za nchi ya Burundi C.7779A Toyota Surf mali ya mgombea ubunge wa Chadema Jeremia Mshandete.
Aliongeza kuwa ndani ya gari hilo pia kulikutwa vifaa vya uhalifu ambavyo ni mapanga 9,vipande vya nondo nane,kombeo tatu na mawe 10.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo kamanda Kamugisha alisema dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina la Charles na vijana wengine waliokuwa ndani ya gari walikimbia baada ya kubaini kuwa wanafuatiliwa na jeshi la polisi.
“Tumepata taarifa kuwa mgombea huyu wa ubunge alikuwa ameandaa kundi la vijana kufanya vurugu wakati wa uchaguzi,aliandaa pombe(viroba) na silaha hizi ili kuwaumiza wananchi hasa wapinzani wake CCM”,aliongeza Kamugisha.
“Watu hawa walikuwa na nia mbaya ya kuumiza watu kwa silaha hizi na pombe kuwapa vijana wakati na baada ya uchaguzi,tayari tunamshikilia Jeremia Msandete na tumejipanga vyema kuhakikisha zoezi la uchaguzi linamalizika salama katika mkoa wa Shinyanga”,alieleza Kamugisha.
Vipande vya nondo na mapanga yanayodaiwa kuwa ni ya mgombea ubunge jimbo la Solwa mkoani Shinyanga Jeremia Mshandete wa Chadema,ni miongoni mwa silaha za jadi zilizokatwa ambazo zinadaiwa kuwa ziliandaliwa kwa ajili ya kufanya uhalifu wakati na baada ya uchaguzi mkuu 2015-
Mawe na makombeo yanayodaiwa kuwa ya mgombea ubunge wa Chadema Jeremia Mshandete
Pombe/Viroba,makombeo na bendera ya CCM
Mapanga,makombeo,mawe na viroba vilivyokamatwa
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akionesha bendera ya CCM iliyochanwa
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga akionesha makombeo yanayoadaiwa kuwa yalilenga kutumika kufanyia vurugu kwenye jimbo la Solwa-
Kamanda Kamugisha akizungumzia kuhusu pombe kali aina ya Vodka
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akionesha panga
Kamanda Kamugisha akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo jioni mjini Shinyanga
Kamanda Kamugisha akizungumza
Kamanda Kamugisha akisisitiza juu ya umuhimu wa wananchi kulinda amani ya nchi katika uchaguzi mkuu 2015-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog