Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mkazi
wa Chang’ombe Emmanuel William (35) kwa tuhuma za
kupiga nyimbo za mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha
Chadema, Edward Lowassa kwa kutumia simu ya mkononi
wakati akiwa kwenye foleni ya wapiga kura.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda
wa Polisi Mkoani hapa, David Misime, alisema mpiga kura
huyo alikamatwa katika kituo cha kupigia kura cha
Chang’ombe mjini hapa Jumapili.
Pia Misime alisema wamewakamata watu watatu katika
kituo cha kupigia kura cha Mbabala wakigawa vipeperushi vya aliyekuwa mgombea ubunge
kwa tiketi ya Chadema, Benson Kigaila.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Emmanuel Pascal (20), Samwel Joseph
(50) na Amos Lugonya (29).
Katika tukio jingine Misime alisema waliwakamata watu watatu katika kituo cha kupigia kura
cha Emaus waliokuwa wamelewa na wakifanya fujo kwenye kituo hicho.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Kizitto Kabwe (36), Masonga Baraka (40) na Benedict
Mbijima (35).
Misime pia alisema katika kituo cha Hamvu, Chamwino walikamatwa wakazi wawili wa
Chang’ombe wakifanya fujo katika kituo cha kupigia kura cha Hamvu.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Tumaini Frank na Seleman Ally.
Kamanda huyo alisema mafaili ya watuhumiwa hao wote yamepelekwa kwa wakili wa serikali
kwa ajili ya kuandaa mashtaka.
Hata hivyo, Misime alisema pamoja na kukamatwa kwa watu hao hali ni shwari mkoani hapa
na watu walishiriki na kupokea matokeo ya uchaguzi kwa amani bila bughudha yoyote.