Mgombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia chama cha APPT– Maendeleo, Elisiana Tabwe, amewataka Watanzania wasipoteze bahati ya kutomchagua mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tabwe alimmwagia sifa Lowassa kupitia Chadema juzi wakati wa mdahalo wa wagombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini uliofanyika Ngokolo na kuandaliwa na Radio Faraja mjini humo kuwa Lowassa ndiye Rais anayefaa kuongoza nchi.
“Ndugu zangu, najua mtanishangaa, lakini bila kumung’unya maneno wala kushinikizwa na yeyote, nawaombeni katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, mkamchague mgombea urais Lowassa, kiongozi ambaye mnatambua utendaji wake wa kazi,” alisisitiza Tabwe. Hata hivyo, mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, na mgombea wa CCM, Steven Masele, walikacha mdahalo huo.