Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ametoa
muda kwa wala rushwa nchini kutubu dhambi zao kabla hajawa
rais na watakaofanya hivyo alishawasamehe saba mara sabini
lakini baada ya hapo akiingia Ikulu “atalala nao mbele”.
Dk Magufuli ambaye juzi alitamka kuwa atawafunga kwa
makufuli mafisadi wote akiingia Ikulu, jana akiwa Kongwa mkoani Dodoma alisema kitendo cha
baadhi ya watu kuendelea kula rushwa na kuwanyonya watu wa hali ya chini kinamkera na
hayuko tayari kuendelea kuona hali hiyo ikiendelea.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, mgombea huyo
alisema ndani ya Serikali kuna watu wachache ambao wanaendelea kutokuwa waaminifu na
akasema hali hiyo ni kasumba na mtu wa aina hiyo hata akipewa mshahara wa Sh20 milioni kwamwezi bado atakuwa ni tatizo.
“Mimi sikuomba urais kwa majaribio, nipeni kazi hii niwashughulikie, walarushwa wote naomba
waanze kutubu mapema lakini wakichelewa hadi Oktoba 25, nitalala nao mbele na hakutakuwa na
msamaha wala kumhamisha mtu kama kaharibu mahali, atabaki hapo akiwa hana kazi,” alisema.
Akizungumzia kero kubwa ya Wilaya ya Kongwa, alisema amechoka kuzika watu wasiokuwa na
hatia, hivyo akiwa rais atahakikisha viongozi wote wanawajibika na wasipofanya hivyo
atawafukuza.
Dk Magufuli alikuwa akizungumzia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji wilayani
Kiteto ambako watu kadhaa wamekwishauawa.
Alisema wakuu wa mikoa, wilaya, makamanda wa polisi na maofisa tarafa katika maeneo husika
wanatakiwa kukaa mguu sawa kwani siku yakitokea mauaji kwenye maeneo yao, basi watatakiwa
kuachia ngazi.
Alieleza kushangazwa kwake na mauaji hayo kuwa ya upande mmoja zaidi hasa
kwa wakulima na kusema muda umefika kama wakulima wataendelea kuuawa basi ng’ombe za
waliosababisha vifo hivyo wataliwa kwenye misiba.
“Wakulima nataka mlime sana hata usiku limeni tu na nyinyi wafugaji nataka mfuge kwa bidii na
kama maeneo hayatoshi basi mtambue kuwa rais ndiye mwenye mamlaka ya kutoa ardhi na
kutenga kwa matumizi mengine ili muweze kunufaika, nitafanya hivyo,” alisema.
Aliwataka wanachama wa Chadema kumpa kura za kutosha ili awasaidie wananchi wa Kibaigwa
kuondoa kero za ushuru mdogo mdogo pamoja na kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili
maisha ya Watanzania yabadilike.
Ahadi nyingine aliyotoa ni kusimamia mikataba kwa madereva wa magari na matreka ili nao
waboreshe maisha yao ikiwamo pensheni kwa wastaafu kwa kuwa waliitumikia nchi kwa uadilifu.
Akiwa wilayani Mpwapwa, aliahidi mambo mawili makubwa ikiwamo ujenzi wa barabara ya lami
kutoka Chipogolo kupitia Gulwe hadi Mbande na kurudisha chuo cha utafiti wa mifugo ambacho
ni cha muda mrefu lakini siku za hivi karibuni kilitangazwa kuhamishiwa mjini Dodoma.
Mgongano CDA
Akiwa mjini Dodoma, Dk Magufuli alisema atashughulikia mgongano wa masilahi ambao
umekuwapo kati ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na manispaa. Alisema
CDA imekuwa hailipi fidia inayostahili kutokana na sheria na kwamba endapo atapata ridhaa ya
kuongoza nchi, atapiga marufuku mamlaka hiyo kuchukua ardhi ya mtu yoyote bila kulipa fidia
inayostahili.
Alisema endapo atapata nafasi hiyo, atajenga viwanda kulingana uzalishaji wa mazao kwenye eneo
husika.
Amtetea aliyehama Chadema
Katika tukio jingine, Dk Magufuli alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime
kuwashughulikia watu wote wanaomtumia ujumbe wa vitisho aliyekuwa meneja kampeni wa
mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema Dodoma Mjini, Khalid Zoya aliyejiunga na CCM.
Alitoa agizo hilo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri.
“Ameniambia kuwa ameanza kupokea ‘meseji’ za vitisho… Najua RPC una utaalamu wa
kushughulika na hili na bahati nzuri wewe ni mtendaji mzuri,” alisema Dk Magufuli huku akisogea
kwa Misime.
Akizungumza katika mkutano huo, Zoya aliahidi kuzunguka katika kata zote za Jimbo la Dodoma
Mjini kuhakikisha kuwa Dk Magufuli na mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Anthony Mavunde
wanachaguliwa. Akizungumzia kuhama kwa Zoya, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Dodoma,
Jella Mambo alisema: “Si jambo geni kuhamahama vyama, alikuwa CCM akaja Chadema sasa
amerudi CCM tunamtakia kila la kheri.”
na Habel Chidawal
