Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limezima mitambo yake mitatu kati ya minne ya kuzalisha nishati katika
bwawa la Kidatu, mkoani Morogoro, ikiwa ni siku moja imepita
tangu ilipotangaza kuzima mashine zake zilizopo kwenye bwawa
la Mtera huko Dodoma.
Akizungumza suala hilo leo, meneja wa kituo cha kuzalisha
umeme cha Mtera, Mhandisi Abdallah Ikwasa amesema mitambo hiyo imezimwa zaidi ya wiki moja baada ya kina cha maji kinachohitajika katika bwawa hilo kupungua hivyo mitambo hiyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Naye meneja wa Kituo cha uzalishaji cha Kidatu, Mhandisi
Justus Mtolera amewaambia wanahabari waliotembelea kituo hicho leo kuwa sababu ya kuzima mashine hizo ni kutokana na kina cha maji kupungua kwenye bwawa hadi kufikia ujazo wa mita
441.88 badala ya 450 kutoka usawa wa bahari.
"Kupungua kwa kina cha maji katika bwawa la Mtera kumetuathiri kwa kiasi kikubwa kwani bila Mtera, Kidatu haiwezi kufanya kazi na mara nyingi tunategemea maji kutoka katika bwawa hilo
lenye uwezo mkubwa ili kuendesha mitambo yetu kwa ufanisi.
"Pia tunategemea maji kutoka katika mito ya Iyovu na Lukosi lakini siyo kwa kiasi kikubwa tofauti
na Mtera. Na hali ikiendelea hadi kufikia mita 433 za ujazo, tutalazamika kuzima hata hii mashine moja inayofanya kazi sasa hivi," amesema Mhandisi Mtolera.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mtolera, bwawa hilo limejaa maji katika ujazo wa mita 450 lina uwezo
wa kuzalisha umeme zaidi ya megawati 200 kwa mashine zote nne kufanya kazi. Lakini hivi sasa
wamelazimika kuzalisha megawati 27 hadi 30 kwa mashine moja.
Ameongeza kuwa chanzo cha hali hiyo kutokea ni mabadiliko ya tabia ya nchi na utunzaji wa mazingira. Hata hivyo, amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwani
serikali inafanya jitihada za kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika kupitia sekta ya gesi badala
ya vyanzo vya maji.