Watu wapatao 200 wameteketeza kwa moto vifaa vya kupiga kura huku wengine wakiwajeruhi wasimamizi wa uchaguzi kwa kile kinachoonekana kuwa ni hofu ya kusambazwa kwa kura feki.
Katika tukio lililotokea wilaya ya Sumbawanga, watu hao wanadaiwa kuteketeza vifaa mbalimbali yakiwamo makasha 45 ya kuhifadhia kura wakidai kuwa yalikuwa na kura ambazo tayari zilikuwa zimeshapigwa .
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa tukio huo katika kijiji cha Zimba , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga .
“Niko njiani nikielekea katika eneo la tukio ni kweli limetokea usiku wa kuamkia leo ….. vifaa hivyo vilikuwa vikisafirishwa kwenda tarafa ya Milepa Bonde la Ziwa Rukwa “ alisema
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mwaruanda alidai kuwa watu wapatao 200 wakiwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga , marungu , mawe na mikuki waliweka vizuizi vya mawe makubwa barabara kijijini Zimba na kulizuia gari lililokuwa likisafirisha vifaa hivyo vya kupiga kura kwenda Tarafa ya Milepa.
Alieleza kuwa gari hilo lenye namba za usajiri T 865 BEU likiwa na maofisa wawili wasaidizi wa uchaguzi na dereva lilizuiliwa na watu hao wenye hasira na kuchoma vifaa vyote vya kupigia kura ambapo watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi .
Kwa mujibu wa Mwaruanda hakuna mtu yeyote waliokuwa wakisafiri katika gari hilo aliyereruhiwa katika tukio hilo ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja .
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Sumbawanga , Adam Missana akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu amekiri kutokea kwa tukio hilo huo akidai ulitokea katika kijiji cha Zimba kati ya saa tatu na nne usiku wa kuamkia leo .
Missana ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Sumbawanga alidai kuwa watu hao wenye hasira wameteketeza kwa kuchoma moto vifaa vyote vya kupigia kura zikiwemo karatasi za kupigia kura wagombea wa urais, ubunge , na udiwani .
“Vifaa vilivyoteketezwa kwa moto ni pamoja na masanduku ya kuhifadhia kura yapatayo 45 , taa , kalamu , karatasi za wagombea urais , ubunge na madiwani “alisisitiza
Akifafanua aliongeza kuwa baada ya kusambaza vifaa vya kupigia kura katika Kata ya Zimba walipofika katika kituo cha mwisho ilikiwa tayari ni saa kumi na mbili jioni askari waliokuwa wakisindikiza gari hilo waligoma kuendelea na safari kwa madai kuwa wangefika Kata ya Milepa usiku .
“Hata hivyo Msimamizi Msaidizi Jimbo, Charles Mwita aliwaasa askari polisi waendeleee na msafari lakini walikataa hivyo gari hilo liliendelea na msafari kuelekea Tarafa ya Milepa bila kuwa na ulinzi wa askari polisi hadi walipo vamiwa na watu hao ambao waliweka vizuizi vya mawe barabarani kijijini Zimba “ alisisitiza .
Aliongeza kueleza kuwa gari hilo lilipofika kijijini Zimba watu wenye hasira walililizua wakiwa na silaha mbalimbali za jadi “walishusha vifaa vyote vya kupigia kura kutoka garini wakanyonya mafuta kutoka kwenye gari hilo kisha wakayatumia kuchomea vifaaa hivyo “alisisitiza
“Maofisa Wasaidizi wa Uchaguzi wawili na dereva wa gari hilo lililotekwa wamejeruhiwa na kuporwa simu zao na vitu vingine vya thamani “ alidai Missana .
Kwa mujibu wa Misaana gari hilo licha ya kuwa na maofisa wasaidizi wa uchaguzi wawili na wakitoka kwenye mafunzo ambao baada ya gari hilo kutekwa walifanikiwa kukimbia kusikojulikana .
Alieleza kuwa baada ya kuwasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) uchaguzi utakao fanyika leo katika Kata ya Milepa ni wa Uraisi tu kwa kuwa kwa taratibu za tume uchaguzi wa Rais hauwezi kuahirishwa .