Afikishwa mahakamani kwa kumtukana Rais Kikwete na Ridhiwani Kikwete

Mkazi wa mjini Moshi, Kyefa Joachim Makundi (33), jana alipandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya  Kikwete.

Mbali na shitaka hilo, mshitakiwa huyo alisomewa shitaka lingine la kumtukana Ridhiwan Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze aliyemaliza muda wake.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga na kusomewa mashitaka hayo na wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Agatha Pima.

Wakili Pima alidai mahakamani kuwa Oktoba 17 mwaka huu katika baa ya Harambee iliyopo katikati ya mji wa Moshi, mshitakiwa alitumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Kikwete na mwanae Ridhiwan.

Ingawa matusi hayo hayakuandikwa kwenye hati ya mashitaka, lakini wakili Pima alidai kitendo hicho ni kinyume cha kifungu 89(1) (a) cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Chini ya kifungu hicho, mtu yeyote anayetumia lugha ya matusi, kuudhi, au kudhalilisha dhidi ya mtu mwingine katika hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani anatenda kosa la jinai.

Adhabu inayotolewa kwa mtu anayepatikana na hatia katika kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela.

Hata hivyo, mshitakiwa alikana shitaka hilo ambapo mahakama ilisema dhamana ilikuwa wazi ikiwa mshitakiwa atakuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh1.5 milioni kila mmoja.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo