MABAO ya Amissi Tambwe na Malimi Busungu yamemaliza uteja wa klabu ya Yanga kwa Simba kwa miaka miwili, kwani ushindi wa mwisho ulipatikana Machi 18, 2013
Katika mchezo wa mwisho wa Yanga kushinda walipata ushindi kama waliopata leo wa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Didier Kavumbagu anayeichezea Azam FC kwa sasa na Khamis Kiiza ambauye leo amevaa jezi ya Simba.
Tambwe ndiye alikuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo dakika ya 44 akimalizia kazi nzuri ya Donald Ngoma aliyemtengenezea mfungaji baada ya kupokea krosi ya Kelvin Yondani.
Kipindi cha pili Simba walirudi kwa kasi ya kusaka bao la kusawazisha lakini Busungu alikata mzizi wa fitna baada ya kukwamisha bao la pili akimalizia mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite kwa kichwa kilichomshinda kipa Peter Manyika JR.
Kwa matokeo hayo Yanga wanaongoza ligi wakiwa na pointi 12 baada ya kushinda michezo minne ya kwanza, huku Simba ikibaki na pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu zilizopita.